Ramaphosa:Afrika Kusini haikuipelekea silaha Urusi
4 Septemba 2023Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema tume ya uchunguzi imegundua hakuna ushahidi kwamba Afrika Kusini ilipakia silaha au risasi katika meli ya Urusi mwezi Desemba mwaka uliopita. Akizungumza jana jioni katika hotuba yake kwa taifa Ramaphosa alisema hakuna madai yoyote yaliyothibitishwa kuwa ya kweli na wale walioyatoa hawawezi kuyathibitisha madai yao.
Ramaphosa alikuwa akizungumzia madai ya balozi wa Marekani aliyesema mapema mwaka huu kwamba serikali ya Afrika Kusini ilikuwa ikiipelekea silaha na risasi Urusi itumie katika vita vyake dhidi ya Ukraine. Balozi huyo alisema silaha hizo inadaiwa zilisafirishwa kupitia meli ya Urusi iliyotia nanga katika kambi ya jeshi la majini karibu na mji wa Cape Town Desemba mwaka jana.
Rasmi Afrika Kusini imetangaza msimamo wa kutoegemea upande wowote katika vita vinavyoendelea nchini Ukraine. Ramaphosa alianzisha uchunguzi kuhusu suala hilo baada ya upinzani katika bunge la Afrika kusini kusisitiza. Ramaphosa amesema serikali inapanga kutoa mukhtasari wa matokeo ya uchunguzi wa tume, lakini sio ripoti kamili kutokana na usiri wa taarifa za kijeshi.