Rangoon. Wito watolewa kufanya maandamano duniani kupinga utawala wa kijeshi wa Burma.
4 Oktoba 2007Makundi ya haki za binadamu yametoa wito wa kufanyika siku ya maandamano duniani kupinga matumizi makubwa ya nguvu dhidi ya maandamano ya amani nchini Burma. Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch yamejiunga na shirika la Crisis Action katika wito wa kuchukuliwa hatua Jumamosi ijayo kuhusiana na matumizi ya nguvu yaliyotumiwa na utawala wa jeshi nchini Burma, ambapo kiasi cha watu 13 wameuwawa na zaidi ya wengine 1,000 wamekamatwa.
Matukio yatafanyika katika nchi kadha ikiwa ni pamoja na Australia , Canada, Ufaransa, India , New Zealand , Uingereza na Marekani. Utawala wa kijeshi wa Burma umeongeza mbinyo dhidi ya watu wake jana Jumatano , ukionya kuwakamata watu zaidi baada ya msako uliofanyika wiki iliyopita, wakati umoja wa Ulaya ukikubali kimsingi kuwaadhibu watawala hao wa kijeshi kwa kuwawekea vikwazo.