1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ranil Wickremesinghe achaguliwa kuwa rais wa Sri Lanka

20 Julai 2022

Wabunge nchini Sri Lanka wamemchagua kaimu rais Ranil Wickremesinghe kuwa rais mpya wa nchi hiyo na kutarajia uzoefu wake serikalini utasaidia kuliokoa taifa hilo kutokana na uchumi unaodorora na mzozo wa kisiasa.

Sri Lanka Colombo | Premierminister Ranil Wickremesinghe
Picha: Eranga Jayawardena/AP/picture alliance

Wickremesinghe ambaye amehudumu kama waziri mkuu kwa mihula sita, alipata kura 134 katika bunge la wanachama 225 licha ya hasira ya umma dhidi ya viongozi baada ya miezi kadhaa ya uhaba mkubwa wa mafuta, chakula na dawa. Ushindi huo wa Wickremesinghe ulikuwa wa kumuondolea lawama baada ya kushindwa katika uchaguzi wa mwaka 2020 kwa chama chake cha United National Party, moja ya vyama vikuu na vya zamani zaidi nchini humo ambao ulimuacha kuwa mbunge wa pekee wa chama hicho bungeni.

Kwa msaada wa chama tawala cha Rajapaksa, Wickremesinghe alijipatia kura 134 zaidi ya mshindi wa pili Dullas Alahapperuma, waziri wa zamani anayeungwa mkono na upinzani aliyejipatia kura 82. Baada ya ushindi huo, Wickremesinghe alisema kuwa taifa hilo linakabiliwa na changamoto nyingi na wanahitaji kufanyia kazi mkakati mpya wa kutimiza matarajio ya wananchi.

Hata hivyo, kiongozi huyo ni mtu asiyependwa na umma uliochoshwa na uhaba wa chakula, mafuta na dawa na wakosoaji wanahoji iwapo anaweza kupata uungwaji mkono wa umma kutekeleza majukumu yake.

Gotabaya Rajapaksa - Aliyekuwa rais wa Sri LankaPicha: Andy Buchanan/AP Photo/picture alliance

Kabla ya uchaguzi huo, wabunge wachache walikuwa wamesema hadharani kwamba watampigia kura Wickremesinghe kutokana na chuki ya wazi dhidi yake, lakini wabunge wengine watiifu kwa chama tawala cha Rajapaksa walitarajiwa kumuunga mkono kwa sababu alikuwa amewahakikishia kwamba atawaadhibu vikali waandamanaji walioyashambulia makazi ya wanasiasa wakati wa ghasia hizo.

Waandamanaji washtushwa na kuchaguliwa kwa Wickremesinghe

Mwitikio wa waandamanaji ulizimwa kwa kiasi kikubwa huku takriban watu 100 tu wakikusanyika katika malango ya makao makuu ya rais lakini wengine wakiapa kugeuza mtazamo ili kumuondoa Wickremesinghe. Mwandamanaji mmoja Damitha Abeyrathne amesema kuwa wameshtushwa na kuchaguliwa kwa Wickremesinghe na kwamba kiongozi huyo ni mtu anayeshughulikia mambo kwa njia ya ujanja. Ameongeza kuwa Wickremesinghe ataanza kuwadhibiti kwa njia tofauti na kama waandamanaji, wataanza tena mapambano. Baadhi ya maelfu ya watu waliojitokeza katika maandamano ya wiki iliyopita ya kulazimisha kuondolewa madarakani kwa rais Gotabaya Rajapaksa, pia walitaka Wickremesinghe aondoke madarakani na kumtaja  kuwa mshirika wa familia ya Rajapaksa.