1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rasimu ya makubaliano ya COP30 yazima juhudi za nishati mpya

21 Novemba 2025

Brazil inayoshikilia Urais wa COP30, imewasilisha rasimu ya pendekezo la makubaliano la mkutano huo wa UN na kuondoa pendekezo la kuunda mpango wa kimataifa wa kuachana na matumizi ya nishati ya visukuku.

Brazil  Belém 2025 | Picha ya pamoja ya wajumbe wa COP30
Wajumbe wanaohudhuria mkutano wa COP30 nchini BrazilPicha: COP 30 Press Office/Anadolu Agency/IMAGO

Katika pendekezo hilo lililowasilishwa mapema leo, maneno yote yanayotaja nishati ya visukuku yameondolewa, lakini pendekezo hilo ambalo bado linapaswa kujadiliwa zaidi, litahitaji kuidhinishwa kwa makubaliano ya pamoja ili liweze kupitishwa.

Suala hilo limekuwa moja kati ya masuala yenye utata zaidi katika mkutano huo wa wiki mbili ulioshirikisha takriban viongozi wa serikali 200 katika mji wa Belem nchini Brazil.

Pendekezo hilo lilikuwa limepingwa vikali na zaidi ya nchi 30 ambazo zilitia saini kwa pamoja barua iliyoandaliwa na Colombia iliyosema kuwa hawewezi kuunga mkono matokeo ambayo hayajumuishi muongozo wa utekelezaji wa haki, utaratibu na usawa katika kuachana na matumizi ya nishati hiyo inayochafua mazingira.

Kulingana na mjumbe aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, China, India, Saudi Arabia, Nigeria na Urusi zimekataa pendekezo hilo la nishati ya visukuku.

Wajumbe watofautiana kuhusu ufadhili

Wajumbe pia wanatofautiana juu ya shinikizo la nchi zinazoendelea za kuyataka mataifa yaliyoendelea kutoa ufadhili zaidi kusaidia mataifa yanayokabiliwa na hatari zaidi kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na kutumia nishati mbadala.

Rachel Cleetus kutoka Muungano wa Wanasayansi Wanaojali, ameiambia AFP kwamba ukosefu wa ufadhili kutoka kwa mataifa tajiri, sehemu muhimu ya Mkataba wa Paris, bado ni changamoto inayoendelea  katika siku hizo za mwisho katika kupata matokeo mahiri na yenye haki.

Na kwa mara ya kwanza katika mkutano wa COP, suala la biashara limekuwa pia la kipaombele.

Wanaharakati wa mazingira wafanya maandamano nje ya ukumbi wa mkutano wa COP30 mjini Belem nchini Brazil Novemba 10, 2025Picha: Igor Mota/ZUMA/picture alliance

Umoja wa Ulaya unapambana na upinzani unaoongozwa na China na India wa kodi ya kaboni kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje kama vile chuma, alumini, saruji na mbolea, hatua ambazo Uingereza na Canada pia zinajiandaa kuchukuwa.

Wajumbe katika mkutano huo wa COP30 leo wanaendelea na vikao vyao baada ya tukio la kuhofisha hapo jana wakati moto ulipowaka kupitia dari la ukumbi wa mkutano huo na kulazimisha kuondolewa kwa haraka kwa waliokuwemo ndani.

Waziri wa utalii wa Brazil Celso Sabino,  amethibitisha kuwa hakukuwa na majeruhi

"Katika dakika chache tu, tukio hili lilitatuliwa. Hakuna ripoti za mtu yeyote aliyejeruhiwa, uokoaji ulifanyika mara moja. Eneo hilo lina milango mingi ya kutokea kwa dharura, hivyo kuwe na uhakika, hili haliharibu taswira ya COP hii, ambayo imekuwa na mafanikio makubwa.

Hilo lilikuwa tukio la tatu kubwa tangu mkutano huo kuanza katika kiwanja cha COP30, kilichoko kwenye eneo la uwanja wa ndege wa zamani lililoundwa kwa mahema makubwa, pamoja na majengo ya kudumu.

Ingawa COP30 inatazamiwa kuhitimishwa leo Ijumaa, mara nyingi mikutano hiyo ya hali ya hewa hurefushwa na kwa kuzingatia muda uliopotezwa jana Alhamisi, huenda pia ukachangia hali hiyo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW