Ratiba ya Kombe la dunia 2014
1 Agosti 2011Rais wa shirikisho la kandanda duniani, FIFA, Sepp Blatter amesema kuwa nchi mwenyeji wa mashindano ya kombe la dunia mwaka 2014 Brazil, inapaswa kuwajibika, kuhakikisha kuwa mshindano hayo yanawacha mrithi akisisitiza kuwa mashindano hayo sio sarakasi tu inayoweka kambi na baadaye kuondoka bila ya kutambulika.
Haya Blatter aliyesema siku moja baada ya kutolewa mpangilio wa timu kwenye mashindano hayo na ameongeza kuwa anaamini Brazil itachukuwa jukumu la kuhakikisha kuwa viwanja katika miji wenyeji, 12 ,vipo tayari kwa wakati unaohitajika na inakabiliana na miundo mbinu duni ya usafiri nchini humo.
Brazil ambayo ni bingwa mara tano wa mashindano hayo iliandaa mshindano hayo mwisho mnamo 1950 na Blatter anakumbuka wakati huo alikuwa ni kijana wa miaka 14 wakati nchi yake Switzerland ilitoka sare na wenyeji hao.
Haya yote aliyasisitiza ni katika jithada pia za kuisafisha sifa ya FIFA ambayo katika miezi ya hivi karibuni imekumbwa na shutuma za ufisadi.
Mpangilio wa timu
Ama kuhusu mpangilio wa timu mbalimbali kwenye mashindano hayo, tunaanza na Ujerumani ambapo timu hiyo ya taifa ya wanaume imeorodheshwa kwenye kundi C, ikiwa pamoja na Sweden, Ireland, Austria, visiwa vya Faroe na Kazakhstan. Naibu kocha Oliver Bierhoff ameeleza kuwa Ujerumani ambayo ni mshindi mara tatu wa mashindano hayo, ipo tayari kwa mipambano hiyo.
Akizungumza na waandishi habari punde tu baada ya kutolewa mpangilio huo mjini Rio de Janeiro, alikokwenda kumwakilisha kocha Joachim Löw, Bierhoff, amesema anaamini kuwa timu hiyo itafanikiwa katika jukumu hilo kama ambavyo imefanikiwa siku za nyuma.
Ameongeza ni jambo zuri kwa wachezaji wa Ujerumani kupata fursa kucheza dhidi ya timu ya Ireland, na kuwa timu hiyo pinzani inapaswa kuwa na motisha na akili tulivu.
Bierhoff anatambua kuwa Ireland ni timu ilio jiimarisha kimchezo, ina wachezaji wazuri, ambao huenda wakafanya mpambano huo kuwa wenye ushindani mkali, lakini anasema hili ndilo jambo linalochangamsha mchezo.
Mapokezi
Hisia nyengine zilizotolewa kuhusu mpangilio wa timu katika mashindano hayo zimetoka kwa kocha wa timu mwenyeji Brazil, Mano Menezes, ambayo timu yake imefuzu moja kwa moja kwenye mashindano hayo, na amesema kuwa lengo lake kwenye timu hiyo ni kukitayarisha kikosi kilicho na nguvu iwezekanayvo kupambana na timu yoyote ile itakayofuzu kwa mashindano hayo.
Kocha wa Uingereza Fabio Capello aliyeshuhudia mpangilio huo mjini Rio, anasema anadhani timu yake inapaswa kuwa na tahadhari. Imepangwa na Moldova ambayo anasema na timu rahisi kukabiliana nayo, lakini timu nyingine katik kundi H walikopangwa wao, Ukraine , Poland na Montenegro anasema anatarajia kuwa kivumbi kitatifuka.
Kwa Afrika,
Na homa hii haipo Ulaya tu na katika nchi nyengine za magharibi bali pia barani Afrika, ambapo miamba ya soka magharibi mwa Afrika, Ghana na Côte D'Ivoire zimepewa kibarua kigumu wakati mpangilio wa kufuzu timu za Afrika kwenye mashindano hayo ya kombe la dunia nchini Brazil ulipotolewa.
Ghana iliyofungwa kwenye robo fainali kupitia mikwaju ya penalti na Uruguay katika mashindano ya mwaka uliopita nchini Afrika kusini, inakabiliana na Zambia, na Sudan pamoja na Lesotho au Burundi katika mojawapo ya timu 10 ya kiwango cha pili.
Cote d'Ivoire ikitafuta kushiriki mara ya tatu kwenye mashindano haya ya kombe la dunia, imaenguka na timu ambayo kila mtu alikuwa haitaki, Morocco, katika ligi ndogo inayokamilishwa na timu ya Gambia na Chad au Tanzania.
Ama kwa upande wa timu ya Nigeria, imeorodheshwa pamoja na Malawi,Ushelisheli au Kenya na Djibouti au Namibia. Algeria inaonana na Mali na Benin ambazo ni timu mbili zenye matokeo duni na imo pia Eritrea au Rwanda.
Mabingwa mara saba wa Afrika, Misri ambayo imewahi kufuzu mara mbili tu kwenye mashindano hayo ya kombe la dunia, inapambana na Guinea katika ligi ndogo na kujumuisha pia Zimbabwe na visiwa vya Comoro au Msumbiji.
Senegal na Uganda ni miongoni mwa timu zilizoendelea barani Afrika na zinalazimika kushindana na Angola na Mauritius au Liberia kwa nafasi ya raundi ya tatu.
Mechi ya mkondo wa kwanza ya awamu mbili inatarajiwa kuchezwa Novemba 11 na 15 na timu 10 za mkondo wa pili zitapambana Juni mosi mwaka ujao, na timu tano za raundi ya tatu, itakayoamua nani anayeshiriki mashindano hayo ya kombe la dunia nchini Brazil, zimepangiwa kuchezwa katika mwezi wa Oktoba na Novemba 2013. Orodha ya Kalenda kuelekea mashindano hayo, imekamilika.
Mwandishi: Maryam Abdalla/Rtre/Afpe
Mhariri:Abdul-Rahman