1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ratiba ya Kombe la Soka la Dunia yaanza kuchemsha

Mohamed Dahman5 Desemba 2009

Mambo tayari yamejiweka kwa kabumbumbu la Kombe la Dunia mwaka 2010 baada ya kutangazwa kwa makundi manane ya timu zinazomenyana katika michuano hiyo ya kwanza kabisa kufanyika Barani Afrika.

Rais wa Shirikisho la Soka la Italia ,Giancarlo Abete (kushoto) akikabidhi Kombe la Dunia kwa Rais wa FIFA Joseph Blatter (kulia), wakiangaliwa na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini (katikati), wakati wa kupangwa kwa kubahatisha ratiba ya mechi za FIFA Kombe la Dunia 2010 mjini Cape Town, Afrika Kusini ,tarehe 04 Desember2009.Picha: picture alliance / dpa

Kilichobakia sasa ni kujinowa na kutembeza ndimi itakuwaje na nani anategemea nini na nani anasema nini.

Liwe kundi la kifo au la hakuna upangaji rahisi ,mechi moja itafanyika kwa wakati mmoja na makocha 32 wa timu za taifa watakuwa wanatafutwa kwa udi na uvumba.

Iwapo wenyeji wa michuano hiyo ya Kombe la Dunia Afrika Kusini wanatazamia miujiza yoyote ile baada ya kupangwa katika kundi gumu la Ufaransa Uruguay na Mexico ambayo ndio itakayofunguwa dimba nayo hapo Juni 11 inaweza kujipa moyo kutokana na ushindi wa Uingereya mwaka 1966.

Wakati ilipokuwa mwenyeji wa michuano hiyo miaka 43 iliopita Uingereza ilitoka sare na wapinzani hao hao wake watatu katika michuano ya kund la awali. Timu hiyo ilitoka sare ya 0-0 na Uruguay kabla ya kuzifunga Mexico na Ufaransa kwa 2- 0 kila timu na hatimae kuja kutawazwa mabingwa wa soka wa dunia.

Afrika Kusini ingeliridhika tu kusonga duru ya pili na kuepuka kuwa timu ya kwanza mwenyeji kufungishwa virago duru ya kwanza ya michuano hiyo. Licha ya kundi lake hilo A kuwa gumu kocha wa timu hiyo Alberto Parreira amejipa moyo kwa kusema kwamba kundi lao pekee katika michuano hiyo yote ile ndio lenye mabingwa wawili wa dunia wa zamani yaani Ufaransa na Uruguay.

Fabio Capello wa Uingereza naye anafahamu kwamba mmjowapo wa muadhara mkubwa katika historia za Kombe la Dunia umetokea mwaka 1950 wakati timu goi goi ya Marekani ilipowabwaga Uingereza kwa 1-0 Kocha huyo amesema safari hii Uingereza haina nafasi ya kubweteka ikiwa katika kundi la Marekani, Algeria na Slovenia.

Maoni kama hayo yametolewa na kocha wa mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia Italia Marcello Lippi ambaye anajuwa fika juu ya balaa fulani la Kombe la Dunia wakati Italia ilipotolewa nje ya michuano hiyo kwa 1-0 na Korea Kaskazini hapo mwaka 1966.

Safari hii hatari inatoka kwa vikaka vinavyotisha mno vya Paruguay,Slovenia na New Zealand.Paraguay kwa muda mrefu ilikuwa ni timu ya Marekani Kusini yenye kuingia Kombe la Dunia kwa ulaini kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Brazil.

Brazil mabingwa wa Kombe la Dunia mara tano kundi lake lina kazi pevu ambapo linajumuisha Ureno,Ivory Coast na Korea Kaskazini.Kocha wa Brazil Carlos Dunga amesisimshwa na timu za kundi lake akisema kwa dhihaka kwamba michuano ya kundi hilo inazikutanisha Brazil A na Brazil B akimaanisha wachezaji nyota akina Decco,Pepe na Leidson wanaochezea Ureno licha ya kwamba wamezaliwa Brazil Uhispania pia iko katika kazi pevu ya kutoana kijasho na timu za Swirtzerland,Hoduras na Chile.


Argentina imewekwa pamoja na Nigeria, Ugiriki na Korea Kusini.Timu zote mbili Argentina na Nigeria hazichekani zote zimeingia kwa meno michuano hii ya Kombe la Dunia.

Katika kundi lake Ujerumani bingwa wa Kombe la Dunia mara tatu itakabiliwa na shinikizo kubwa la kushinda mechi zake kutoka sio tu nyumbani bali pia ulimwenguni kwa jumla timu hiyo itakwaruzana na Australia,Ghana na Serbia.Ghana inatambuliwa kuwa ni timu nzuri ambapo hapo mwaka 2006 ilingia duru ya pili ya michuano ya Kombe la Dunia licha ya kwamba kundi lake lilikuwa na timu ngumu za Italia,Jamhuri za Czech na Marekani.


Ivory Coast tayari imelaani bahati yao kwa kupangwa kile walichokiita kundi la G la kifo hasa kuwa kuwepo Brazil na Ureno ukiachilia Korea Kaskazini.

Mabingwa mara nne wa Afrika Cameroon ina kibarua cha kutolaza damu kwa kuwekwa na vigogo wa soka wa Ulaya Uholanzi na Denmark na Japani.


Kwa hiyo bongo limeanza kuchemka na halitosita hadi hapo fungua dimba ya michuano hiyo ya Kombe la Dunia kati ya Afrika Kusini na Mexico hapo tarehe 11 Juni mwakani.


Mwandishi: Mohamed Dahman /dpa /REUTERS

Mhariri:Mtullya,Abdu Said