1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raundi ya mtoano ya 16 bora Champions League kuanza

14 Februari 2022

Jumanne, Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya, Champions League, inaanza tena kurindima huku zikichezwa mechi za duru ya muondoano ya kumi na sita bora.

UEFA Champions League Spanien  Real Madrid-Inter Milan.
Picha: Colas Buera/PRESSINPHOTO/picture alliance

Mechi itakayotupiwa jicho na wengi ni mchuano kati ya Real Madrid na Paris Saint Germain.

Ndoto ya PSG ya kushinda taji lao la kwanza la Champions League inakabiliwa na kikwazo kwa mara nyengine watakapopambana na vinara wa La Liga Madrid ambao wameishinda hiyo ligi ya mabingwa mara 13 na kuweka rekodi.

Msimu wote huu PSG imekuwa na wakati mgumu inapopambana na timu zinazofanya mashambulizi ya kushtukiza ya haraka na Madrid kwa sasa inacheza mchezo wa aina hiyo. Madrid yenyewe lakini haijatinga fainali ya Champions League tangu mwaka 2018 iliponyakua taji la tatu mfululizo la mashindano hayo.

Lionel Messi akisherehekea goli lake na mchezaji mwenzake Juan BernatPicha: Federico Pestellini/PanoramiC/imago images

Na sasa kocha wao Carlo Ancelotti anaelekea kupambana na timu ya zamani aliyoifunza ambayo inapitia kipindi kigumu kwa sasa kwani imeshinda mara moja katika mechi nne za mashindano yote inayoshiriki.

Mbali na mechi hiyo RB Salzburg watakuwa wanapambana na mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich kisha Sporting Lisbon wachuane na vinara wa ligi Kuu ya England Manchester City. Mechi nyengine ya kusisimua itakuwa kati ya Intermilan na Liverpool huko Sansiro.

Mechi nyengine za mkumbo wa kwanza wa raundi ya kumi na sita bora zitachezwa katikati ya wiki ijayo Chelsea wakipambana na Lille, Juventus wawe wenyeji wa Villareal nao Manchester United waelekee Uhispania kucheza na Atletico Madrid nao Ajax Amsterdam wapambane na Benfica huko nchini Ureno.