RB Leipzig yakataa kusalimu amri
2 Novemba 2016Kwa upande wa mabingwa Bayern Munich hali hiyo ilitarajiwa. Kwa upande wa Leipzig ambayo imepanda daraja msimu huu na Hoffenheim ambayo ni timu ya kijijini hilo halikutarajiwa. Kwa upande wa Hoffenheim mafanikio yanaweza kuwekwa mabegani mwa kocha kijana kabisa katika Bundesliga , Julian Nagelsmann, akiwa na umri wa miaka 29. Kikosi chake kilionesha ukomavu mkubwa katika mpambano dhidi ya Hertha BSC Berlin na kupata ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na mlinzi wa kati Niklas Suele ambaye anasema alitamani sana kufunga bao kwa muda mrefu na sasa ametimiza ndoto yake. Huyu hapa Sule.
Nilitamani sana kufunga bao. Ilichukua muda. Kwa hiyo ni bao muhimu sana kwangu na lilikuwa muhimu sana kwa timu yetu. Tumefanikiwa leo kwa kuonesha mchezo mzuri sana. Wote tumefurahi, kwamba tumeweza kupata hapa nyumbani pointi tatu. Hilo lilikuwa muhimu sana.
FC Kolon ilipata ushindi wa mabao 3-0 jana Jumapili , na inaendelea kubaki juu katika msimamo wa ligi. Mshambuliaji wa Kolon Antony Modeste alipachika mabao yote matatu jioni ya jana na kuongoza orodha ya mafungaji mabao katika Bundesliga akiwa na mabao 11 katika michezo 9, akifuatiwa nyuma na Robert Lewandowski wa bayern Munich na Pierre Emerick Aubamiyang wa Borussia Dortmund. Mchezaji wa FC Kolon Simon Zoller anasema. "Nafikiri , kwamba msimu huu tuna kila fursa ya kushangilia. Nafikiri leo, kwa msingi wa kipindi cha pili , tumestahili matokeo hayo. Kwa kuwa Hamburg walikuwa na wachezaji pungufu uwanjani tulitumia vizuri fursa hiyo na kupata mabao matatu, ambapo mwishoni ni ushindi tuliostahili pia.
RB Lepzig sio tu haijafungwa msimu huu , lakini pia inashangaza kila mtu kwa kuwa timu inayoifuata Bayern Munich katika nafasi ya pili. Timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu ilishinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Darmstadt siku ya Jumamosi. Wageni hao katika Bundesliga tayari imejikusanyia pointi 21 na inabakia katika nafasi ya juu karibu na Bayern Munich ambayo ina pointi 23. Tulikuwa na kibarua kigumu sana ambacho tulikitekeleza kwa ustadi mkubwa sana, amesema kocha wa Leipzig Ralph Hasenhuttl. Mshambuliaji wa Leipzig Timo Werner alikuwa na haya ya kusema. "Tulistahili ! nafikiri , katika sehemu ya kipindi cha kwanza tulionesha wazi. Pengine hatukuweza kupata fursa ya kulazimisha kupata bao, lakini tulitawala. Naamini katika kipindi cha kwanza tulipata bao la kuongoza, kwa kuwa tulifunga bao , na halikuwa la kuotea. Na ndio sababu hata mwisho wa mchezo kwa ushindi huu tulistahili. Bayern Munich haikufanya makosa na kuibamiza tena Augsburg kwa mabao 3-1. Katikati ya wiki timu hizo zilikutana katika kombe la shirikisho DFB Pokal na Bayern ilishinda kwa idadi hiyo hiyo ya mabao.
Katika pambano la watani wa jadi Borussia Dortmund na Schalke 04 hakuna mbabe. Mchezo huo uliochezwa katika uwanja wa Signal Iduna Park uliishia sare ya bila kufungana. Mlinzi wa Schalke 04 Benedikt Howedes kuhusu pambano hilo la watani wa jadi anasema. "Tunaridhika na matokeo ya mchezo huo. Katika kipindi cha kwanza , nadhani , tulifanya vizuri. Tulipata fursa nzuri zaidi za kufunga bao. Katika kipindi cha pili Dortmund ilikuja juu, na nafikiri katika vipindi vyote kwa kiasi fulani tulifanya vizuri."
Leverkusen ilipata ushindi dhidi ya VFL Wolfsburg , na Freiburg ikapata ushindi wake wa kwanza ugenini dhidi ya SV Werder Bremen. Vipigo hivyo kwa Werder Bremen na hasa Wolfsburg vimeibua mjadala mpya wa makocha wa timu hizo. Wolfsburg ilimtimua kocha wake wa muda mrefu Dieter Hecking na kumpa kazi hiyo kocha wa timu ya vijana wa timu hiyo Valerien Ismail ambaye hajaipatia timu hiyo uwezo wa kushinda , ikiwa imepata ushindi mara moja tu na kufungwa mara tano na sare tatu. Bado Wolfsburg inaendelea kusaka kocha atakayeipatia timu hiyo uwezo wa ke tena wa kushinda. Kuna tetesi kwamba Wolfsburg imeanza mazungumzo na kocha Andre Villas Boas ili kuinoa timu hiyo. Bremen hali kadhalika bado inasubuka kutoka katika janga la kupoteza michezo ikiwa imepoteza michezo 6, sare moja na ushindi mara mbili.
Low arefusha mkataba wake na timu ya Ujerumani
Wakati huo huo kocha Joachim Loew aliyeiletea Ujerumani kombe la dunia amerefusha mkataba wake na shirikisho la kandanda nchini Ujerumani DFB. Loew mwenye umri wa miaka 56 , ambaye amekuwa kocha wa timu ya taifa Die Mannschaft , tangu mwaka 2006 na kupata ushindi wa kombe la dunia mwaka 2014, amesema majadiliano kuhusiana na mkataba mpya na shirikisho hilo yamekwenda vizuri na hakukuwa na sababu ya kutorefusha mkataba huo.Rais wa shirikisho hilo alisifu kazi ya Loew katika timu ya taifa na kusema ni kocha bora kabisa ambae tunaweza kumfikiria.Loew ambaye mkataba wake ulikuwa unaishia mwaka 2018 katika kombe la dunia nchini Urusi, ataendelea kufanyakazi na benchi lake la ufundi hadi mwaka 2020.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre
Mhariri: Yusuf saumu