Real Madrid, Atletico Madrid kukutana tena
21 Machi 2015Mabingwa hao watetezi, ambao walizabwa magoli manne kwa sifuri na Atletico mwezi uliopita, walipangwa katika mchuano huo utakaokuwa marudio ya fainali ya mwaka jana. Pia, bingwa wa 2013 Bayern Munich atapambana na FC Porto, Paris Saint-Germain itashuka dimbani na Barcelona, wakati Juventus wakimaliza kazi dhidi ya Monaco.
Madrid ilitwaa kombe hilo mwaka jana kwa mara ya kumi - (La Decima) ilipoishinda Atletico mabao manne kwa moja. Atletico na Real Madrid zitapambana kwa mara ya saba na nane msimu huu, huku Real ikishindwa kupata ushindi wowote. Mchuano wa mkondo wa kwanza utachezwa Aprili 14, huku wa marudiano ukiwa Aprili 22. Fainali ya mwaka huu itakuwa katika uwanja wa Olimpiki mjini Berlin Juni 6.
PSG haitakuwa na mshambuliaji wake mkuu katika mkondo wa kwanza uwanjani Parc des Princes baada ya Zlatan Ibrahimovic kuonyeshwa kupigwa marufuku kucheza mchuano mmoja kufuatia kadi nyekundu aliyoonyeshwa dhidi ya Chelsea katika duru iliyopita.
PSG iliizaba Barca 3-2 nyumbani katika hatua ya makundi lakini ikashindwa 3-1 uwanjani Camp Nou. Timu hizo pia zilikutana katika robo fainali misimu miwili iliyopita, huku Barca ikifuzu kwa faida ya mabao ya ugenini.
Baada ya kutinga robo fainali kwa mara ya 14, Bayern inapigiwa upatu tena kuizidi nguvu Porto ambayo iliwanyamazisha mabingwa hao wa Ujerumani katika fainali ya Kombe la Ulaya mwaka wa 1987. Porto ilishinda kombe hilo mwaka wa 2004 chini ya Kocha Jose Mourinho kwa kuwazaba Monaco.
Juventus, ambayo imetinga robo fainali kwa mara ya pili katika misimu mitatu, ilitaka kuepuka Bayern. Sasa ni kama matumainin yake yako juu baada ya Kupewa Monaco.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo