Real Madrid kukwaruzana na Bayern Munich
23 Aprili 2014Pambano la leo linafuatia mchezo wa kwanza wa nusu fainali nyengine jana kati ya Chelsea ya Uingereza iliokuwa ugenini mjini Madrid kuumana na Athletico Madrid , mchuano uliomalizika sare bila kwa bila na hivyo kusubiriwa mchezo wa marudiano mjini London wiki ijayo.
Usiku huu Real Madrid ambayo imeshalinyakua kombe la Ulaya mara 10 itakuwa ikicheza nyumbani, wakati Bayern Munich ambayo imelitwaa taji hilo mara tano ikijaribu kulitetea tena , baada ya kutawazwa mabingwa msimu uliopita. Madrid itawategemea zaidi nyota wake wanne, Christiano Ronaldo, Karim Benzema , Angel Di Maria na Garith Bale.
Kikosi cha Bayern chini ya Mwalimu Pep Guardiola wakiwemo Frank Ribbery , Arjen Robben ,Mario Goetz na Philipp Lahm , kitamkosa mchezaji wa kiungo Bastian Schweinsteiger. ambaye alipewa kadi nyekundu katika pambano la robo fainali dhidi ya Manchester United ya Uingereza.Timu hizo mbili Bayern Munich na Real Madrid zimeshawahi kukutana mara tano katika nusu fainali na mara nne ni Bayern ilioibuka na ushindi.
Wahenga wanasema mramba asali harambi mara moja-Bila shaka Bayern Munich inawania kurudia tena ilichokifanya msimu uliopita iliponyakua mataji matatu, Ubingwa wa ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga, kombe la vilabu bingwa barani ulaya Champions league na Kombe la kilabu bingwa ya dunia.
Jee leo katika pambano hilo la kwanza la nusu fainali itakuaje, tusiandikie mate na wino upo. Kwa jumla asiye na mwana aeleke jiwe na asiye na mguu basi atie gongo, muamuzi ni kipenga cha mwisho.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, afp. dpa
Mhariri: Saumu Yusuf