1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Real Madrid na Napoli zatinga Robo fainali, Champions League

16 Machi 2023

Timu nane zitakazoshiriki robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya zimebainika rasmi. Hii ni baada ya kuchezwa jana usiku mechi mbili za mwisho za mkondo wa pili wa hatua ya 16 bora.

Champions League | Real Madrid vs FC Liverpool
Picha: Denis Doyle/Getty Images

Mabingwa watetezi Real Madrid wamefuzu kuingia robo Fainali baada ya kuicharaza Liverpool ya Kocha Jurgen Kloop bao 1-0 katika uwanja wa Santiago Bernabeu. Bao hilo lilitiwa nyavuni na mchezaji mahiri na mshindi wa Ballon d´Or Karim Benzema katika dakika 78, na hivyo Madrid kusonga mbele wakiwa na jumla ya mabao 6-2.

Liverpool walionekana kuzidiwa kabisa na hivyo kushindwa kuubadili mchezo kama walivyofanya dhidi ya Barcelona mwaka 2019 au dhidi ya AC Milan kwenye fainali ya mwaka 2005. Madrid sasa wameiondoa Liverpool kwenye Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kwa misimu mitatu mfululizo, ikiwa ni pamoja na kuitoa katika fainali ya mwaka jana.

Soma pia: Man City na Inter Milan zatinga robo fainali, Champions League

Ilikuwa ni mechi ya 300 kwa Real Madrid katika michuano hii ya Ligi ya Mabingwa, Ulaya. Mlinda lango wa Liverpool Alisson Becker na yule wa Real Madrid Thibaut Courtois wote walionyesha mchezo mzuri.

Katika mechi nyingine, Napoli wamefuzu kuingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza katika historia yao baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Eintracht Frankfurt. Victor Osimhen alifunga mabao mawili na Piotr Zielinski akaongeza bao jingine kwa mkwaju wa penalti. Napoli imefuzu kwa ushindi wa jumla ya mabao 5-0.

Vurugu za mashabiki mjini Napoli kabla ya mechi

Vurugu mjini Napoli, Italia za mashabiki wa Eintracht Frankfurt na Napoli (15.03.2023)Picha: CIRO FUSCO/ANSA/AFP

Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha maafisa wa polisi wakishambuliwa kwa kurushiwa meza, viti na baruti katikati maeneo ya jiji hilo la Italia. Angalau gari moja la polisi lilichomwa moto. Likinukuu vyanzo vya polisi, shirika la habari la ANSA lilisema kuwa mashabiki wa timu zote mbili za Frankfurt na Napoli walishiriki katika vurugu hizo.

Awali, mashabiki wa Klabu ya Frankfurt walikuwa wamepigwa marufuku ya kuingia nchini humo na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Italia, lakini walishinda rufaa na kuwasili kwa wingi mjini Napoli ambapo walianza kwa maandamano ya amani kabla ya vuruga kuzuka na kusababisha uharibifu mkubwa.

Hatimaye polisi wa Italia walifanikiwa kuwadhibiti mashabiki hao wa Frankfurt na kuwapakiza kwenye mabasi hadi kwenye hoteli zilizo katika eneo la bandari. Wakati wa msafara huo, mabasi hayo yaliripotiwa kushambuliwa na mashabiki wa Napoli kwa kurushiwa mawe na chupa.

Soma pia:Liverpool, Madrid kuumana Ligi ya Mabingwa 

Meya wa Napoli Gaetano Manfredi amesema wanalaani kwa nguvu zote vitendo hivyo visivyoelezeka na wale waliohusika bila kujali ni wa upande gani, huku akisisitiza kuwa matukio ya uharibifu katika mji wao wa kihistoria hayakubaliki.

Timu hizi nane ndio zimefuzu kuingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Champions League: Real Madrid, Napoli, Manchester City, Inter Milan, Bayern Munich, Chelsea, Benfica na AC Milan. Sasa, washiriki watasubiri kufahamu watapangwa na nani katika droo itakayofanyika Ijumaa (17.03.2023) mjini Nyon, Uswisi.