Real Madrid yaipiku Barcelona na kunyakua ubingwa wa La Liga
20 Julai 2020Msimu wa kandanda wa Uhispania ulimalizika jana Jumapili(19.07.2020) ambapo Real Madrid , Sevilla na Granada zikiwa miongoni mwa washindi wakubwa na Barcelona , Valencia na Espanyol wakiwa washindwa wakubwa. Imeonekana wazi kwamba zile timu zilizofanya vibaya zaidi zilimtimua kocha angalau mmoja katika msimu uliovurugika kwa miezi kadhaa kutokana na janga la virusi vya corona na kumalizika bila ya mashabiki.
Zinedine Zidane ameiongoza Real Madrid katika ubingwa wake wa 34 wa la Liga katika siku ya mwisho ya msimu kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Villarreal. Karim Benzema alifunga mabao hayo mawili na mabao yake jumla 21 yalikuwa muhimu kwa timu hiyo. Sergio ramos amemaliza wa pili kwa ufungaji katika klabu hiyo msimu huu akiwa na mabao 12 na huenda Real wakampatia mkataba mwingine kupindukia 2021 wakati mkataba wake wa sasa utakapomalizika.
Leonel Messi amepat tuzo yake ya saba ya ufungaji mabao mengi katika La Liga jana baada ya kupachika mabao mawili katika kichapo cha mabao 5-0 cha Barcelona dhidi ya Alaves katika duru ya mwisho.
Messi amepachika mabao 25, manne zaidi ya Karim Benzema.