Real Madrid yajiimarisha kileleni Uhispania
30 Januari 2017Madrid walitanua uongozi wao kileleni na tofauti ya pointi nne na bado wana mchuano wa kucheza zaidi ya wapinzani wao. Real Madrid iliifunga Real Sociedad 3 - 0 katika mchuano ambao Cristiano Ronaldo licha ya kufunga bao moja alizomewa sana na mashabiki wa Real. CR7 ndiye anayeonekana kunyooshewa kidole cha lawama kutokana na matokeo mabaya ya Real ambapo wameshinda mechi moja tu kati ya nne na hata wakatolewa katika Kombe la Mfalme dhidi ya Celta Vigo. Mapema jana, Barcelona walitoka sare ya 1-1 na Real Betis na wakasonga katika nafasi ya pili baada ya Sevilla nao kuchabangwa 3-1 na Espanyol. Real wana pointi 46, Barca ni wa pili na 42 pointi sawa na nambari tatu Sevilla na faida ya mabao.
Lakini matokeo ya Barca yalimwacha kocha Luis Enrique na hasira baada ya bao lao kukataliwa na refarii licha ya kuonekana kuvuka mstari wa lango.
Kocha Enrique ametoa wito wa uongozi wa kandanda la Uhispania kuzindua matumizi ya teknolojia ya kubaini kama mpira umeingia wavuni au la.
Tennis
Na katika tennis, Roger Federer alitwaa ushindi dhidi ya mpinzani wake wa muda mrefu Rafael Nadal katika fainali ya tisa ya grand slam iliyowakutanisha magwiji hao wawili wa tennis. Mpambano huo wa fainali ya Australian Open mjini Melbourne kwa upande wa wanaume ilitajwa kuwa kubwa kabisa kuwahi kuchezwa katika mchezo huo wa tennis.
Lilikuwa ni taji lake la 18 la grand slam, na lake la kwanza katika kipindi cha miaka mitano. Mswisi huyo mwenye umri wa miaka 35 alimpiku Mhispania Nadal kwa seti za 6-4, 3-6, 6-1, 3-6, 6-3. Ushindi huo ulimpandisha hadi nafasi ya kumi katika orodha ya wachezaji bora duniani.
Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Yusuf Saumu