Real Madrid yamtimua kocha Carlo Ancelotti
26 Mei 2015Kocha huyo raia wa Italia, aliiongoza Madrid kutwaa taji la kombe la Uhispania kabla ya kuisaidia klabu hoyo kunyakua taji la kumi la klabu bingwa barani Ulaya – UEFA Champions League ambalo lilipewa jina maarufu la La Decima.
Pamoja na mafanikio hayo aliyoyapata msimu uliopita, mwaka huu haukuwa mzuri kwa vijana hao wa Santiago Bernabeu baada ya kushindwa kutwaa hata kombe moja licha ya kuwa klabu hiyo tajiri ilifanya usajili wa hali ya juu wa wachezaji nyota.
Mambo yalizidi kuwa mabaya baada ya klabu hiyo kubanduliwa nje na Juventus ya Italia katika hatua ya nusu fainali ya klabu bingwa barani Ulaya huku wapinzani wao wakubwa Barcelona wakinyakuwa taji la ligi kuu Uhiapania La Liga, na kutinga fainali ya klabu bingwa na kombe la Mfalme – Copa Del Rey.
Rais wa Madrid Florentino Perez amewaambia waandishi wa habari kuwa haikuwa rahisi kumtema kocha huyo ambaye alimshukuru kwa huduma zake. Perez amesema kocha mpya atateuliwa wiki ijayo huku wachambuzi wakibashiri kuwa kocha wa Napoli ya Italia, Rafa Benitez huenda akaijaza nafasi hiyo.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu