Real Madrid yataka majibu kufuatia fujo wakati wa fainali
3 Juni 2022Mechi hiyo ambayo Madrid iliibuka na ushindi wa 1-0, ilicheleweshwa kwa zaidi ya dakika 30 baada ya maafisa kuwazuia watu waliokuwa wakijaribu kuingia kwa nguvu katika uwanja wa Stade de France. Polisi wa kukabiliana na ghasia walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya mashabiki, wakiwemo wanawake na watoto.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Gerald Darmanin amesema mashabiki wa Liverpool ndio wanafaa kubebeshwa lawama kubwa, na kwamba kulikuwepo kati ya mashabiki 30,000-40,000 waliofika bila ya tiketi halali, hali iliyosababisha msongamano mkubwa wa watu waliokuwa wakijaribu kuingia uwanjani kwa nguvu.
Hata hivyo mashabiki wa Liverpool wameipinga hoja ya waziri Darmanin kwamba wao ndio wanafaa kubeba dhamana kwa fujo lililozuka katika uwanja wa Stade de France, badala yake wakisema wengi wao walikuwa na nidhamu japo polisi wa kutuliza ghasia wa Ufaransa ndio walitumia nguvu kubwa kuzuia mashabiki.
Darmanin amekiri kuwa polisi ya Ufaransa ililemewa na mamia ya watu aliowaita "wahalifu" ambao walijitokeza kuzua ghasia.
"Tunataka kujua ni sababu zipi zilizochochea fujo nje ya uwanja na vigezo gani vilitumika kuthathmini kilichotokea siku hiyo," klabu hiyo ya La Liga imesema katika taarifa.
"Pia tunaomba majibu na maelezo ili kubaini waliohusika na kuwaacha mashabiki bila ya uangalizi. Nidhamu ya mashabiki wetu ilikuwa ya hali ya juu kila wakati. Kama ilivyoonekana katika picha zilizochapishwa kwenye vyombo vya habari, mashabiki wengi walishambuliwa, kunyanyaswa na kuibiwa."
Real Madrid imesema mashabiki wao wanastahili majibu juu ya kilichotokea wakati wa fainali ya ligi ya mabingwa. Mkurugenzi mtendaji wa Liverpool Billy Higan ametaka kufanyike uchunguzi juu ya matukio hayo, akielezea kuwa mashabiki wote wa Liverpool na Real Madrid walipitia hali ngumu.
Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA limeamuru uchunguzi huru juu ya tukio hilo, wakati waziri wa michezo wa Ufaransa Amelie Oudea-Castera akisema Jumatatu kwamba watatoa ripoti yao ndani ya siku 10.