RENAMO kusaini mkataba wa mwisho wa amani
6 Agosti 2019
Hili ni jaribio la tatu la kutafuta suluhisho la kudumu kati ya serikali na RENAMO tangu mwaka 1992.
Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Filipe Nyusi na kiongozi wa chama cha RENAMO, Ossufo Momade, kusaini makubaliano katika bustani ya kitaifa ya Gorongosa, baada ya kukubaliana rasmi kumaliza uhasama wa kijeshi baina yao.
Makubaliano hayo yalihitimisha harakati za muda mrefu za kutafuta amani zilizoanzishwa na Afonso Dhlakama, kiongozi wa muda mrefu wa chama cha RENAMO aliyefariki dunia Mei 2018 na yalijiri miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 15.
Zaidi ya wapiganaji 5,200 wa RENAMO, wanatarajiwa kurejesha silaha zao kwa serikali, lakini chama hicho bado kinakabiliwa na migawanyiko ya ndani.
Kundi dogo ndani ya chama hicho cha upinzani ambacho awali kilikuwa vuguvugu la waasi, limeapa kutorejesha silaha zao na kukataa kumtambua kiongozi wake mpya, Momade.