1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Republican wa Ufaransa wamjadili Fillon

Mohammed Abdulrahman
6 Machi 2017

Viongozi wa ngazi ya juu wa chama cha Republican cha Ufaransa wanakutana kumjadili mgombea wao wa urais, Francois Fillon, anayeandamwa na uwezekano wa kushindwa, huku binafsi akisema suala la kujiondoa halipo.

Frankreich Wahlkampf Francois Fillon in Aubervilliers
Picha: picture-alliance/abaca/L. Christian

Pamoja na kuwaomba radhi Wafaransa kwa tuhuma za kudanganya kuwa alimuajiri mkewe Penelope na watoto wao wawili kushughulikia kazi zake za kibunge na kuwalipa maelfu ya euro, bado Fillon anashikilia mkewe alisimamia kazi zake kadhaa.

Katika moja ya mahojiano aliyowahi kufanyiwa Bibi Penelope binafsi miaka ya nyuma, alieleza kuwa hahusiki na kazi za kisiasa za mumewe, lakini katika mahojiano na gazeti la Journal du Dimanche la kila Jumapili, sasa amebadili kauli akisema alifanya kazi za kumsaidia mumewe.

Jana (Machi 5), vigogo wa chama cha Republican walitangaza wangelikutana leo jioni kuzungumzia suala la Fillon kuendelea kuwa mgombea. Mkutano huo, hata hivyo, hautohudhuriwa na waziri mkuu wa zamani, Alain Juppe, aliyeshindwa na  Fillon katika mbio za mchujo za kutafuta mgombea wa chama hicho, akimaliza nafasi ya pili.

Juppe,  ambaye alisema hatokubali kuwa mgombea mbadala pindi Fillon atajitoa, anasemekana ameshawishiwa na wanasiasa kadhaa abadili msimamo wake pindi hayo yatatokea.

Vigogo hao wameingiwa na wasiwasi kwamba huenda Fillon asifanikiwe kuingia duru ya pili mwezi Mei, akiangushwa katika duru ya kwanza mwezi ujao na kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, Marien Le Pen, na  mgombea wa kujitegemea anayefuata siasa za wastani, Emmanuel Macron,  wanaopigiwa upatu kuingia duru ya pili mwezi Mei. 

Fillon aapa kusonga mbele
 
Wanasiasa  kadhaa  wameshamuacha mkono Fillon, akiwemo mkuu wa kampeni yake, Patrick Stefanini, na msemaji wake mkuu, Rhierry Solere, ambao wote ni kutoka  chama cha  siasa za wastani za  mrengo wa kulia UDI, kilichotangaza kuwa kinasitisha kwa muda  uungaji mkono wake kwa mgombea huyo.

Wafuasi wa Francois Fillon wanaendelea kujaa kwenye mikutano yake licha ya kuandamwa na kitisho cha kushindwa mgombea wao.Picha: picture alliance/dpa/T. Camus

Akihutubia mkutano mkubwa wa wafuasi wake mjini Paris jana, Fillon  mwenye umri wa miaka 63 aliyekuwa waziri mkuu katika serikali ya rais wa zamani, Nicolas Sarkozy, aliwaambia  wafuasi wake kuwa ataendelea kuwa mgombea na katu hatojiondoa katika mbio hizo.

Katika mkutano huo aliokuwa amezungukwa na wanasiasa kadhaa wa Republican wanaoendelea kumuunga mkono, Fillon alielezea mpango wake aliouita wa "kurejesha heshima ya taifa" hilo.

Hivi leo, Rais Francois Hollande alionya kuwa Le Pen anaweza kushinda uchaguzi ujao wa rais na kusema atafanya kila awezalo kuhaklikisha  anazuwia uwezekano wa mwanasiasa huyo kushika madaraka, akisisitiza kwamba uchaguzi huo utakuwa  juu ya hatima na mustakbali wa Ufaransa kuelekea Ulaya.

Marine Le Pen anayepinga uwanachama wa Ufaransa katika Umoja wa Ulaya amekula kiapo kuwa ataitisha kura ya maoni kuhusu suala hilo, pindi akishinda uchaguzi.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, afp, rtr
Mhariri: Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW