Ribery harudi dimbani hadi Machi
13 Februari 2014Gazeti la kila siku nchini Ujerumani, Bild, limesema mwanamichezo huyo mwenye umri wa miaka 30 anatazamiwa kukosa mechi tatu za Bayern baada ya operesheni ya hapo Alhamisi kurekebisha mshipa mmoja wa damu uliopasuka.
Huku Bayern ikiongoza ligi ya Ujerumani kwa pointi 13, Ribery atakosa mechi mbili za Bundesliga na pia mechi ya Jumatano ya Lgi ya Mabingwa, Champions League, ambapo timu yake itacheza mchezo wake wa kwanza na Arsenal.
Ribery hatarajiwi kurejea uwanjani hadi wakati mechi ya nyumbani dhidi ya Schalke 04 tarehe 1 Machi, endapo tu jeraha lake litakuwa limepona.
Ikiwa jeraha hilo litaleta mashaka yoyote, basi Ribery anaweza kujikuta amechelewa kwa matayarisho ya raundi ya pili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya timu ya Uingereza maarufu pia kama Gunners tarehe 11 Machi.
Mchezaji huyo mwenye asili ya Kifaransa anatazamiwa kuanza mazoezi madogo madogo mwishoni mwa wiki hii, kuanza kukimbia wiki moja baadaye.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman