Rice ziarani Mashariki ya Kati
18 Juni 2005Jerusalem:
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Condoleezza Rice, leo ameanza ziara yake ya kwanza ya Mashariki ya Kati. Ameziomba Israeli na Palestina zishirikiane kwa dhati katika mpango wa Waisraeli wa kuondoka katika Ukanda wa Gaza. Bibi Rice, aliyekwenda moja kwa moja mjini Jerusalem baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa Tel Aviv, atazungumza baadaye leo na Kiongozi wa Wapalestina, Mahmud Abbas mjini Ramallah. Atarudi tena mjini Jerusalem kabla ya kuzungumza na Viongozi mbalimbali wa Israeli pamoja na Waziri Mkuu, Ariel Sharon na Mnadhimu Mkuu mpya, Dan Halutz. Hiyo ni awamu ya kwanza ya ziara yake ya siku sita itakayomchukua hadi Jordan, Misri na Saudi Arabia kabla ya kuhudhuria mikutano ya kimataifa mjini Brussels, Ubelegiji na London, Uingereza.