Richard von Weizsäcker asifiwa kuwa kiongozi bora
2 Februari 2015Gazeti la "Osnabrücker Zeitung" linalozungumzia kifo cha Weizsäcker aliyekuwa rais wa Ujerumani kuanzia mwaka 1984 hadi 1994. Mhariri wa gazeti hilo anamsifu Weizsäcker kwamba alikuwa rais mwenye kuheshimiwa kuliko wote waliomtangulia ama kumfuata. Mhariri huyo anendelea kusema: "Alikubaliwa na wafuasi wa vyama vyote kwa sababu hakuwa mwanasiasa wa kawaida. Alijihusisha katika masuala mengi, kuanzia mambo ya utamaduni, michezo na hata masuala ya dini. Na atakumbukwa hasa kwa hotuba aliyoitoa tarehe 8 mwezi Mei mwaka 1985."
Katika hotuba hiyo ya tarehe 8 Mei Weizsäcker alisema ushindi dhidi ya utawala wa Wanazi ulikuwa pia ukombozi wa Wajerumani. Kwa mtazamo wa gazeti la "Kieler Nachrichten" hotuba ya Weizsäcker aliyoitoa siku ya kumbukumbu ya miaka 40 baada ya kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia ilikuwa hotuba iliyomuweka Weizsäcker juu ya marais wengine wa Ujerumani. Mwaka 1985 baadhi ya Wajerumani bado hawakuwa tayari kutazama kushindwa kwao katika vita vikuu vya pili kwa macho mapya. Bila hotuba ya Weizsäcker, labda Ujerumani mbili zisingeweza kuungana na kuwa nchi moja.
Ugiriki iko njia panda
Gazeti la "Westfälische Nachrichten" linasisitiza kwamba Ugiriki lazima ielewe nchi zinazotumia sarafu ya Euro haziihitaji Ugiriki kwa ajili ya kuiimarisha sarafu hiyo, badala yake, Ugiriki inaihitaji Euro ili uchumi wake usiendelee kudorora na kufikia kiwango cha nchi zinazoendelea. Kama Ugiriki inataka kubakia ndani ya kanda ya Euro, hatua ya kwanza ni kubana matumizi. Hatua ya pili ni kuleta mabadiliko makubwa ya mfumo.
Mhariri wa gazeti la "Der Tagesspiegel" anamkosoa waziri mkuu mpya wa Ugiriki Alexis Tsipras kwa kung'ang'ania nchi yake ipunguziwe madeni. Mhariri huyo anasema: Hilo haliwezekani. Na ikumbukwe kwamba muda unakwenda. Benki kuu ya Ulaya imetishia kwamba itaacha kuipatia Ugiriki fedha mwishoni mwa mwezi huu iwapo nchi hiyo itashindwa kufikia makubaliano na wale walioikopesha.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/Inlandspresse
Mhariri: Saumu Yusuf