Riek Machar afikishwa mahakamani Juba
22 Septemba 2025
Kiongozi wa upinzani na aliyekuwa makamu wa rais nchini Sudan Kusini, Riek Machar amefikishwa mahakamani Jumatatu(22.09.2025) kwa mara ya kwanza akikabiliwa na tuhuma za kuhusika na uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhaini, baada ya serikali kumfungulia mashtaka mwezi huu.
Vyombo vya habari vya serikali Sudan Kusini vimeripoti juu ya kufikishwa mahakamani Machar hatua ambayo imekuja baada ya mwezi huu kufunguliwa mashtaka ya kuhusika na mauaji, uhaini na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Serikali mjini Juba inayoongozwa na rais Salva Kiir ilitangaza juu ya kuchukuliwa hatua hiyo ikisisitiza kwamba kuna ushahidi unaothibitisha kwamba Machar alihusika na kundi la wanamgambo wenye silaha linalojulikana kama White Army.
Joseph Geng Akech waziri wa masuala ya sheria na katiba Sudan Kusini alithibitisha msimamo huo wa serikali kwa kutowa ufafanuzi ufatwao.
"Mnamo March mwaka huu kundi la wanamgambo wenye silaha linafahamika kama White Army lilianzisha mashambulio ya kupanga dhidi ya kambi ya wanajeshi wa Sudan Kusini SSPDF na kusababisha kuuwawa kwa meja jenerali David Majur Dak na zaidi ya wanajeshi 250 na marubani wa Umoja wa mataifa''
Baada ya serikali kutangaza tuhuma hizo,Machar aliondolewa pia kwenye nafasi yake ya umakamu wa rais kwenye serikali ya Umoja wa kitaifa pamoja na kwamba kwa miezi amekuwa chini ya kifungo cha nyumbani.
Makubaliano tete ya kugawana madaraka kati ya rais Salva Kiir na hasimu wake huyo wa muda mrefu yamekuwa yakitetereka kwa miezi sasa na kutishia nchi hiyo kurudi kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha watu 400,000 kuuwawa katika mwaka 2010.
Katika kesi inayomuandama makamu huyo wa zamani wa kwanza wa rais anatuhumiwa kutowa amri kwa wanamgambo kushambulia kambi ya kijeshi mwezi March na kusababisha mauaji ya wanajeshi.
Kambi ya Machar inakanusha tuhuma hizi ikisema ni sehemu ya juhudi za rais Kirr kutaka kuweka kando upinzani na kujichukulia madaraka yote.
Wakili wa Machar ameiambia mahakama hivi leo Jumatatu kwamba mteja wake huyo hapaswi kushtakiwa na mahakama aliyosema haiwezi kuaminika na isiyokuwa na mamlaka.
Ni mara ya kwanza kwa kesi hiyo dhidi ya Machar na maafisa wake wengine kusikilizwa mahakamani mjini Juba.
Wafuasi wa Machar wanasema mashtaka dhidi ya kiongozi huyo yanaonesha dhahiri kwamba mkataba wa kugawana madaraka umekufa na wametowa mwito wa kuchukua silaha na kufanya mabadiliko ya kiutawala.