1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Ripoti: Idadi ya wanaonyongwa Iran yapanda kwa asilimia 25

28 Aprili 2022

Ripoti mpya iliyochapishwa na mashirika mawili ya kutetea Haki za Binadamu imeonesha idadi ya watu walionyongwa nchini Iran mwaka 2021 ilipanda kwa asilimia 25.

Symbolbild Galgen
Picha: Nerijus Liobe/Zoonar/picture alliance

Masharika mawili ya kutetea haki za binadamu ya IHR lenye maskani yake nchini Norway na lile la nchini Ufaransa la ECPM linalopinga adhabu ya kifo yamesema ongezeko la idadi ya watu wanaohukumiwa kifo na kunyongwa nchini Iran inatisha.

Ripoti ya masharika hayo inaonesha utekelezaji wa adhabu ya kunyonga uliongezeka zaidi nchini Iran kuanzia mwezi Juni mwaka jana baada ya kuchaguliwa kwa rais mwenye misimamo ya kihafidhana Ebrahim Raisi.

Ripoti hiyo inasema watu wasiopungua 333 walinyongwa nchini Iran mwaka uliopita, ikiwa ni ongezeko la asilimia 25 ikilinganishwa na watu 267 walionyongwa mwaka 2020. Takwimu hizo zimekusanywa kupitia duru huru za habari na vyanzo rasmi nchini Iran.

Miongoni mwao ni wanawake 17 na idadi kadhaa ya watu kutoka  jamii za wachache nchini Iran.

Idadi ya walanguzi wa dawa za kulevya walionyongwa yaongezeka 

Tangu kuchaguliwa kwa Ebrahim Raisi kuwa rais wa Iran, idadi ya watu wanaonyongwa nchini humo imeongezeka.Picha: WANA/REUTERS

Kadhalika kati ya walionyongwa mwaka jana, 126 walikuwa watu waliotiwa hatiani kwa makosa ya ulanguzi wa dawa za kulevya, idadi ambayo ni kubwa mara tano ya watu 25 walionyongwa kwa makosa hayo mwaka 2020.

Kulingana na masharika hayo idadi hiyo inatia mashaka  kwa sababu tangu mwaka 2017 Iran ilipunguza kwa kiasi kikubwa kuwanyonga watu wanaotiwa hatiani kwa makosa ya biashara ya dawa za kulevya. Hilo lilitokana na mabadiliko ya sheria ya kukabiliana na biashara hiyo haramu baada ya kuwepo shinikizo kubwa la kimataifa.

Karita ripoti hiyo ya leo masharika hayo yametaja pia kuongezeka kwa idadi ya wanawake wanaonyongwa kwa makosa ya kuwauwa wenza au ndugu zao. Wanaharakati wanaamini huenda wanawake hao walinyanyaswa na mauaji yalitokea katika hali ya kujilinda.

IHR na ECPM yataka madola yenye nguvu kuiwekea shinikizo Iran 

Baadhi ya watu hunyongwa hadharani nchini Iran Picha: Loredana Sangiuliano/SOPA Images via ZUMA Press Wire/picture alliance

Mashirika hayo mawili yameyataka mataifa makubwa duniani kuishinikiza Iran kuachana na adhabu ya kifo.

Yamependekeza mataifa yanayoshirika majadiliano ya kuufufua mkataba wa nyuklia na Iran waliweke mezani pia suala la adhabu ya kifo wakisema inatisha kwamba dola hiyo ya Uajemi inashika nafasi ya pili ya duniani baada ya China kwa idadi kubwa ya watu wanaonyongwa kila mwaka.

Kadhalika kuna suala pia la usiri katika utekelezaji wa adhabu hiyo. Karibu asilimia 80 ya adhabu zote za kifo zilizotekelezwa nchini Iran mwaka uliopita hazikutangazwa.

Mkurugenzi wa shirika la IHR Mahmood Amiry-Moghaddam amesema anatiwa mashaka kwamba hakuna shinikizo la kutosha dhidi ya rikodi dhaifu ya haki za binadamu nchini Iran na mataifa makubwa yanawekeza nguvu kujadili suala la mradi tata wa nyuklia bila kulifungamanisha na masuala kama adhabu ya kifo ndani ya Jamhuri hiyo ya kiislamu.