1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti juu ya Umoja wa Afrika.

Zainab Aziz2 Machi 2005

Ripoti ya umoja wa mataifa inasema kuwa Umoja wa nchi za Afrika hauna nguvu za kukabiliana na maasi na mauaji katika jimbo la Darfur nchini Sudan.

Umoja wa nchi za Afrika una jukumu la kusimamisha mapigano, mateso na mauaji yanayo endelea katika jimbo la Darfur lililo kaskazini mwa Sudan.

Lakini Umoja huu wa nchi za Afrika unajikuta katika hali ya kurudi nyuma dhidi ya jukumu hili kutokana na ukosefu wa fedha, utaratibu wa ugavi, vifaa bora vya mawasiliano, vifaa vya kivita na miongoni mwa hayo Umoja wa Afrika hauna fedha za kuwamudu wanajeshi wa kulinda amani.

Hadi sasa kuna nusu tu ya idadi ya wanajeshi kutoka mataifa ya Kiafrika waliofika Darfur kuhudumu kama ilivyo kubalika.

Idadi kamili inayohitajika ni wanajeshi 3320 lakini hali ya kimahitaji ya kibinadamu ya idadi hiyo nusu ya wanajeshi iliyoko Darfur, ni hali ya kusikitisha kutokana na dhiki wanazozipata ni mfano wa kuishi jahanamu ukiwa bado duniani hali hiyo imeelezwa namna hiyo na katibu mkuu wa baraza la umoja wa mataifa bwana Koffi Annan.

Bwana Annan alipokuwa Ulaya mwezi uliopita katika mkutano aliueleza ujumbe wa Umoja wa Ulaya na ujumbe wa NATO kuwa Umoja wa Afrika unahitaji msaada wa dharura ili kuuwezesha kufanikisha malengo yake.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika nchini Sudan balozi Baba Gana Kingibe akilihutubia baraza la usalama la umoja wa mataifa alisema kuwa Umoja wa Afrika unafanya kila jitihada kuona kwamba idadi kamili ya wanajeshi 3320 imeafikiwa na mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika kufikia mwezi aprili mwaka huu.

Lakini akasisitiza kuwa mpango huu utafanikiwa tu iwapo wafadhili watatoa michango yao kama walivyo ahidi zikiwemo Marekani, Umoja wa Ulaya Kanada Netherlands, Uingereza na Ujerumani miongoni mwa mataifa mengine.

Kwa sasa Umoja wa Afrika una jukumu la kupeleka wahudumu wa kulinda amani katika jimbo la Darfur haraka iwezekanavyo hivyo ni sawa na kusema umoja huu unahitaji fedha zaidi, na wahudumu wenye ujuzi.

Msemaji wa shirika moja la misaada la kimataifa ambae hakutaka jiana lake litajwe anasema kuwa tatizo kubwa linaloukabili Umoja wa Afrika ni uongozi bora, mipango muafaka,utumizi wa teknolojia ya habari na ukosefu wa maafisa wahudumu wenye ujuzi kwani maafisa wengi hupenda kujiunga na umoja wa mataifa badala ya Umoja wa Afrika kwa sababu ya tafauti ya mishahara baina ya mashirika haya mawili.

Ameshauri pia Umoja wa Afrika unahitaji kutupilia mbali mila yake ya kuona haya kuomba usaidizi kwani wito wa umoja huo wa `Suluhisho la Matatizo ya Afrika ni Afrika Yenyewe" ni mzuri lakini kivitendo Umoja wa Afrika ungekuwa na uwezo zaidi wa kutatua matatizo yaliyopo kama ungalikuwa na uwezo wa kifedha.

Kwa upande mwingine serikali ya Washington ilikuwa na wakati muafaka wa kusaidia kupatikana kwa haki huko Darfur kama serikali hiyo ingeupa umoja wa Afrika msaada wa kifedha mwezi uliopita lakini badala yake Marekani imepeleka msaada zaidi wa fedha Kusini mwa Sudan.

Baraza la usalama la umoja wa mataifa linadhamira ya kupeleka kikosi cha maafisa wahudumu alfu kumi wa umoja wa mataifa huko kusini mwa Sudan kufuatilia mkataba wa amani uliotiwa saini hivi majuzi baada ya mapigano yaliyodumu kwa miaka 21 shughuli ambayo italigharimu baraza hilo dola billioni moja katika mwaka wa kwanza wa huduma.

Emira Woods, mkurugenzi mwenzi wa taasisi ya maswala ya sera za nje ilyopo Marekani amesema kuwa Umoja wa Afrika hauna uwezo wa kifedha jambo hili litaifanya jamii ya kimataifa ionekane kama inafanya kusudi kutotoa misaada kwa wakati unaofaa ili Umoja wa Afrika ushindwe.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW