1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya Shirika la Oxfam yasema njaa yaongezeka kwa kasi

16 Septemba 2022

Shirika la kimataifa la Oxfam limesema, njaa inaongezeka kutokana na uharibifu wa hali ya hewa ambapo limetoa mwito kwa mataifa tajiri kupunguza uzalishaji wa hewa chafu na yalipe fidia kwa nchi zilizoathirika..

Deutschland G7 Gipfel Protest
Picha: Angelika Warmuth/dpa/picture-alliance

Kulingana na ripoti hiyo ya shirika la Oxfam, hali mbaya zaidi inayosababishwa na uchafuzi wa mazingira inasababisha majanga kama ukame na mafuriko makubwa ambapo maeneo yanayokabiliwa na athari hiyo yanashuhudia kuongezeka kwa majanga hayo pamoja na njaa kali kwa watu wake.

Athari ya ukame inayosababishwa na hali mbaya ya hewa.Picha: CC / Oxfam International

Ripoti hiyo iliyopewa jina la, "Njaa katika ulimwengu wenye joto kali," imesisitiza kuwa baa la njaa limeongezeka kwa asilimia 123 katika kipindi cha miaka sita kwenye mataifa kumi yaliyoathiriwa zaidi, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Mshauri mkuu wa sera ya maswala ya kibinadamu wa Shirika la Oxfam nchini Marekani,  Lia Lindsey, ameliambia shirika la habari la AFP, kwamba "Madhara ya mabadiliko ya tabia nchi tayari yanaonekana. Ameongeza kuwa ripoti hiyo imetolewa ili kuwashinikiza viongozi wa dunia katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wachukue hatua.

Soma:Je mabadiliko ya tabia nchi yamechangia mafuriko?

Nchi zilizokumbwa na hali mbaya ya hewa katika miongo miwili iliyopita ni pamoja na Somalia, Haiti, Djibouti, Kenya, Niger, Afghanistan, Guatemala, Madagascar,Ethiopia, Burkina Faso na Zimbabwe.

Kulingana na ripoti zilizokusanywa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, takriban watu milioni 48 kote katika nchi hizo wanakabiliwa na njaa. WFP imesema idadi hiyo imeongezeka kutoka watu milioni 21 mnamo mwaka 2016 na sasa watu milioni 18 wako hatarini kukabiliwa njaa kali.

Wanyama wanakufa kutokana na ukamePicha: AP

Shirika la Oxfam katika ripoti yake limesisitiza kuwa njaa inayochochewa na hali mbaya ya hewa ni mfano mkubwa unaodhihirisha ukosefu wa usawa duniani huku nchi ambazo hazihusiki na uchafuzi wa hali ya hewa zikiteseka zaidi na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Gabriela Bucher, mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Oxfam, katika taarifa yake ameserma mataifa tajiri kiviwanda kama ya G20 yanawajibika kwa zaidi ya robo tatu katika uzalishaji wa hewa chafu ya kaboni duniani na hivyo amewataka viongozi wa nchi hizo tajiri watimize ahadi zao za kupunguza hewa chafu na amesema ni lazima walipie hatua za kukabiliana na hali hiyo pamoja na hasara na uharibifu katika nchi zenye kipato cha chini. Nchi tajiri zimetakiwa zitoe fedha za kuokoa maisha ya watu haraka ili kukidhi mwito wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzisadia nchi zilizoathirika zaidi.

Nembo ya Shirika la Kimataifa la Misaada la OxfamPicha: AP Graphics

Umoja wa Mataifa umetoa mwito wa misaada ya kibinadamu kwa mwaka huu wa 2022 wa dola bilioni 49, ambazo Shirika la Oxfam limebainisha kuwa ni sawa na faida ya siku 18 ya makampuni ya mafuta ambazo zinahitajika kuwasaidia watu walio hatarini kuangamizwa na njaa.

Bucher, amesema kufuta madeni kunaweza pia kuzisaidia serikali za nchi masikini huku nchi tajiri zikitakiwa kuzingatia jukumu la kimaadili la kuzilipa fidia nchi maskini zilizoathirika zaidi na uchafuzi wa mazingira. Shirika la misaada la Oxfam limetoa wito wa kutozwa ushuru mkubwa kwa makampuni yanayochafua mazingira.

Vyanzo:AFP/DPA

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW