1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhuru wa matumizi ya Intaneti Marekani na Ujerumani washuka

13 Novemba 2025

Uhuru wa matumizi ya mtandao wa intaneti unaripotiwa kuporomoka nchini Marekani na Ujerumani wakati mataifa hayo ya Magharibi yakiungana na nchi zinazoongozwa kimabavu kuweka vikwazo vya kubinya uhuru wa kujieleza.

Mitandao ya kijamii katika simu ya kiganjani
Mitandao ya kijamii Picha: Matthias Balk/dpa/picture alliance

Taasisi hiyo ya utafiti ya ukuzaji wa demokrasia yenye makao yake makuu mjini Washington, imesema kwa ujumla uhuru wa mtandao duniani umeshuka kwa mwaka wa 15 mfululizo, na kupungua kwa nchi ambazo zimeorodheshwa kuwa "huru".

Mwandishi mwenza wa ripoti hiyo Kian Vesteinsson, amesema wameshuhudia "ukandamizaji unaozidi kuwa mbaya katika mataifa ya kiimla na yale ya kimabavu, hasa kwa sababu serikali katika nchi hizo huona kuzuia intaneti na kujieleza mtandaoni kama njia ya kudumisha mamlaka." Ameutaja haswa mwaka 2025 kwamba demokrasia imeshuka.

Amesema kwa bahati mbaya hilo limeonekana kote Amerika ya Kaskazini na Ulaya Magharibi, mwelekeo wa kuzuia uhuru wa kiraia kujieleza katika baadhi ya nchi, na kwa wengine kuongeza vizuizi kwa watu wanaotuma maudhui ya chuki au matatizo.

Mitandao ya kijamii katika simu ya kiganjaniPicha: Yui Mok/dpa/picture alliance

Marekani ilipata alama 73 katika uzani wa uhuru wa intaneti kufikia Mei mwaka huu ikiwa ni kiwango cha chini kabisa na ikishuka kwa pointi tatu kutoka mwaka uliopita. Ripoti hiyo imebainisha kwa sehemu hatua za utawala wa Rais Donald Trumpza kuwakamata watu wasio raia wa Marekani juu ya maoni yao mtandaoni.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, ametishia kuwafukuza watu kutokana na kauli zao juu ya Israel, maamuzi ambayo yanapingwa mahakamani. Ujerumani pia imeshuka kwa alama tatu hadi 74. Kwa mujibu wa taasisi ya Freedom House, Ujerumani imeshuhudia kuongezeka kwa udhibiti binafsi na pia utekelezaji wa sheria zinazozuia matamshi ya chuki na kukashifu.

Imetaja hukumu iliyosimamishwa ya kifungo jela na faini iliyotolewa kwa mhariri wa tovuti ya mrengo mkali wa kulia juu ya chapisho lake kwenye mtandao wa kijamii ambalo lilijumuisha picha iliyochakachuliwa kukosoa mwanasiasa.

Ripoti hiyo pia imetaja kushuka kwa kiwango kikubwa cha uhuru wa intaneti nchini Kenya, ambako mamlaka ilizima mtandao kwa muda mfupi ili kukabiliana na maandamano ya nchi nzima. Nchi nyingine zilizorodheshwa kuwa katika kipengele hicho ni pamoja na Venezuela na Georgia. Tanzania ambayo haikutajwa katika ripoti hii pia ilizima mtandao wa intaneti kwa zaidi ya siku nne kufuatia ghasia za wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.

Tamar Kintsurashvili apata Tuzo ya Uhuru wa Kujieleza ya DW

03:13

This browser does not support the video element.

Serbia imeainishwa kama nchi iliyo "huru kwa kiasi" kutoka kipengele cha nchi "huru" huku Nikaragua ikiwekwa katika orodha ya nchi "zisizo huru" kutoka "huru kwa kiasi."

Bangladesh ilipata mafanikio zaidi, baada ya serikali mpya iliyoundwa kufuatia uasi wa wanafunzi kulegeza vikwazo nchini humo.

Taasisi ya Freedom House, iliyoanzishwa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ili kukuza demokrasia, kihistoria ilikuwa ikifadhiliwa kwa kiasi kikubwa na serikali ya Marekani, lakini iliendeshwa kwa uhuru.

Tangu Rais Trump aliporejea madarakani alipunguza ufadhili kwa mashirika ya haki ikiwa ni pamoja na Freedom House, ambayo imepunguza wafanyakazi.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW