1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroKenya

Urusi imewapeleka zaidi ya Wakenya 1,000 kupigana Ukraine

19 Februari 2026

Zaidi ya Wakenya 1,000 wamekwenda kupigana upande wa jeshi la Urusi nchini Ukraine. Ripoti ya kijasusi iliyowasilishwa katika bunge la Kenya, imesema wengi wa raia hao walidanganywa ili kusaini mikataba ya kijeshi.

Askari wa Urusi wakiwa kwenye eneo la Kursk la Urusi
Urusi inashawishi wanaume kutoka Afrika kwa ahadi za ajira zenye mishahara minono, lakini inawalazimisha kupigana Ukraine.Picha: Russian Defense Ministry Press Service/AP/picture alliance

Uchunguzi mwingi wa vyombo vya habari, ukiwemo ule uliochapishwa mapema mwezi huu na AFP, umefichua jinsi Urusi ilivyowashawishi wanaume kutoka nchi za Afrika kwa ahadi za ajira zenye mishahara minono, na badala yake kuwalazimisha kupigana mstari wa mbele nchini Ukraine.

Uchunguzi wa pamoja uliofanywa na Idara ya Kitaifa ya Ujasusi ya Kenya na Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, uliowasilishwa bungeni Jumanne, ulisema idadi ya walioajiriwa kutoka nchini humo ni "zaidi ya 1,000" -- ikiwa ni juu zaidi kuliko idadi ya "karibu watu 200" iliyotolewa na mamlaka mwezi Desemba. Kiongozi wa serikali bungeni Kimani Ichung'wah amesema Wakenya huondoka nchini kwa kutumia viza ya watalii ili kujiunga na jeshi la Urusi kupitia Instanbul, Uturuki, pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Lakini alisema kuongezeka kwa utekelezaji wa sheria za mpaka katika uwanja wa ndege wa Nairobi kulimaanisha kuwa waajiriwa pia sasa wanasafiri kwenda nchi zingine za Afrika ili kuepuka kugunduliwa. Ichung'wah aliongeza kuwa mashirika ya ajira yasiyo na kibali nchini Kenya "yanashirikiana na wafanyakazi wafisadi wa uwanja wa ndege". Takribani Wakenya 39 wamelazwa hospitalini kwa sasa, 28 hawajulikani waliko na 89 wako vitani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW