Ripoti: Waandishi habari 104 wameuawa mwaka 2024 duniani
10 Desemba 2024Hayo yameelezwa na Shirikisho la Kimataifa la Wanahabari (IFJ) lenye makao yake makuu mjini Brussels, Ubelgiji.
Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Anthony Bellanger, amesema mwaka 2024 umekuwa mbaya zaidi kwa wanahabari ambao wamekuwa wakilengwa moja kwa moja wakati wa mizozo kama unaoshuhudiwa huko Palestina.
Shirikisho hilo la IFJ limeorodhesha pia wanahabari 520 ambao wamezuiliwa gerezani. Maeneo yaliyotajwa kuwa hatari zaidi kwa waandishi wa habari ni Mashariki ya Kati, Asia-Pasifiki na Ulaya hasa kutokana na vita vinavyoendelea nchini Ukraine.
China iliongoza orodha ya nchi zinazowafunga jela waandishi habari ikiwa na wanahabari 135, ikiwemo Hong Kong, ambako maafisa wamekosolewa na mataifa ya magharibi kwa kulazimisha sheria za usalama wa kitaifa zinazokandamiza ukosoaji na uhuru mwingine.