Ripoti: Watoto milioni 8 hawaendi shule Sudan
23 Januari 2026
Kulingana na ripoti ya Save the Children, idadi hiyo ni sawa na zaidi ya watoto milioni nane. Inger Ashing, Mkurugenzi Mtendaji wa Save the Children amesema kwa sasa jumuia ya kimataifa inashindwa kuwasaidia watoto wa Sudan. Ripoti hiyo imesema kuwa idadi hiyo ya watoto wa Sudan wamekosa takribani siku 500 za masomo tangu vita vilipozuka Aprili, 2023.
Ashing amesema idadi hiyo ni zaidi ya iliyorekodiwa wakati wa janga la UVIKO-19, na kwamba shule nyingi zimefungwa au zimeharibiwa katika mzozo huo, huku nyingine zikitumika kama makaazi ya familia zilizoyakimbia makaazi yao. Katika siku za hivi karibuni, mashambulizi ya droni yameongezeka katika mji wa al-Obeid, mji mkuu wa jimbo la Kordofan Kaskazini, na kusababisha vifo vingi vya raia kwa takribani visa viwili.
Save the Children imesema ni asilimia tatu tu ya shule ndiyo zimefunguliwa katika jimbo la Darfur Kaskazini, ambako mzozo bado unaendelea, huku maeneo ya Kordofan Magharibi, Darfur Kusini na Darfur Magharibi, yakiwa pia yamethiriwa vibaya. Baadhi ya walimu wameacha kazi zao, baada ya kutolipwa mishahara kwa miezi kadhaa.
Ripoti ya shirika hilo imebainisha kuwa bila ufadhili wa haraka wa fedha za kuwalipa na kuwafundisha walimu, kurejesha madarasa, na kutoa vifaa muhimu vya kufundishia, mfumo wa elimu uko katika hatari ya kuporomoka kabisa. Ashing amesema elimu ni njia ya kuokoa maisha ya watoto dhidi ya unyonyaji na kuajiriwa katika makundi yenye silaha. Mwezi huu, Ashing alizuru katika shule za Port Sudan, Mto Nile na Khartoum.
Mashirika ya kutoa misaada yametoa wito wa kupatikana msaada wa haraka katika mji wa al-Fashir, ulioko kwenye jimbo la Darfur lililoangukia chini ya udhibiti wa wanamgambo wa RSF tangu mwezi Oktoba, pamoja na Kadugli, mji mwingine uliozingirwa kusini mwa Sudan. Miji yote miwili inakabiliwa na njaa kali.
Wakati huo huo, hospitali mpya iliyokarabatiwa mjini Khartoum imeanza kuwapokea wagonjwa wake wa kwanza, takribani miaka mitatu baada ya kushambuliwa. Hospitali ya Bahri, ilivamiwa na RSF Aprili, 2023, mara tu baada ya mapigano kuzuka kati ya wanamgambo hao na jeshi la Sudan.
Dokta Ali Mohamed Ali, amesema hawakutarajia kama hospitali hiyo itafunguliwa tena. Akiwa mwenye furaha ya kurudi katika wodi yake ya zamani ya upasuaji, Dokta Ali amesema hospitali hiyo iliharibiwa kabisa na hapakuwa na kitu kilichobakia, hivyo iliwabidi waanze tangu mwanzo.
Katika hatua nyingine, shirika la habari la Middle East Eye limesema kuna madai kwamba RSF wamenunua ndege sita za kivita huku kukiwa na upinzani mkali wa kijeshi kati yake na jeshi la Sudan. Katika ripoti yake iliyotolewa Januari 21, shirika hilo limesema ndege hizo ni pamoja na chapa "Sukhoi Su-24 na MiG-25, ambazo kwa kawaida zinatoka Serbia.
Kulingana na Shirika la Habari la Uingereza, BBC, ikinukuu chanzo cha kijasusi cha Sudan ambacho hakikutaka kutajwa jina, ripoti hiyo imesema ndege hizo hugawanywa vipande vipande na kisha kuchukuliwa kwa ndege za mizigo kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu hadi Ethiopia au al-Kufra, kambi ya kikosi cha anga iliyoko mashariki mwa Libya kabla ya kuishia Sudan.
Huku hayo yakijiri, tovuti ya Sudan Tribune imesema kuwa takribani mawakili 16 wameuawa na wengine 32 wametekwa nchini Sudan tangu mzozo ulipoanza miezi 33 iliyopita. Sudan Tribune ilizungumza na Mohamed Salah al-Din, mwanachama wa Chama cha Wanasheria wa Dharura wa Sudan, aliyesema jeshi la Sudan, polisi na idara ya ujasusi wamekuwa wakiwashikilia mawakili, waandishi habari, wanaharakati, madaktari, walimu na raia wengine kwenye maeneo yanayodhibitiwa na jeshi kwa madai ya kuwa na uhusiano na RSF.
(AFP, Reuters)