Ripoti ya HRW yasema mustakabali wa madikteta wazidi kufifia
13 Januari 2022Mkurugenzi huyo amesema katika ripoti ya mwaka huu wa 2022 kwamba watu katika nchi zinazotawaliwa na madikteta wameendesha harakati za kuwania demokrasia kuanzia Cuba hadi Hong Kong. Amesema watu wamejitokeza mabarabarani kudai demokrasia hata katika hatari ya kutiwa ndani au kupigwa risasi. Roth ameongeza kusema kwa vile madikteta hawawezi tena kutegemea chaguzi zinazoendeshwa kwa hila ili kudumisha mamlaka yao, wengi wao sasa wanatumia njama dhahiri ambazo zinahakikisha matokeo wanayotaka lakini matokeo hayo hayatoi uhalali wa uchaguzi.
Bwana Kenneth Roth amesema madikteta wanaweka mbele maslahi yao binafsi kabla yale ya wananchi wao. Hata hivyo ameshauri kwamba viongozi wa nchi za kidemokrasia wanapaswa kutekeleza sera bora zaidi ili kuzikabili changamoto za dunia. Ameeleza kwamba viongozi wengi kwenye nchi za kidemokrasia wametingwa na maslahi ya muda mfupi kwa ajili ya kujipatia mitaji ya kisiasa badala ya kuweka mkazo juu ya maswala muhimu, kama vile ya mabadiliko ya tabia nchi, janga la maambukizi ya virusi vya corona, ubaguzi wa rangi na umasikini. Amewataka viongozi waliochaguliwa kwa njia halali kufanya kazi nzuri ili kuyashughulikia masuala hayo.
Katika dibaji ya ripoti ya mwaka huu ya asasi hiyo ya haki za binadamu mkurugenzi, Kenneth Roth ameyapinga maoni kwamba nchi za madikteta zinastawi wakati zile za kidemokrasia zinafifia. Amesema madikteta wengi wanadai kwamba wanawatumukia watu wao vizuri kuliko viongozi waliochaguliwa kwa njia za kidemokrasia.
Amesema madikteta wanayatumia mapungufu yaliyopo katika nchi za magharibi ili kuwavutia watu wao lakini pia amebainisha makosa ya Marekani na nchi nyingine za magharibi. Amesema Marekani inaendelea kuziuzia silaha nchi kama Saudi Arabia, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu licha ya sera za ukandamizaji za serikali za nchi hizo. Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Human Rights Watch amewata viongozi wa nchi za kidemokrasia kufanya mambo mazuri zaidi badala ya kuzungumzia tu juu ya mapungufu yaliyopo kwenye nchi zinazoongozwa na madikteta.
Chanzo:https://media.hrw.org/preview/en/2266/world-report-2022