Ripoti ya IAEA dhidi ya Iran yagubika mkutano wa kilele wa Teheran
31 Agosti 2012Iran inakabwa na kishindo cha kisiasa hii leo kufuatia ripoti ya shirika la kimataifa la nguvu za atomiki-IAEA inayosema kwamba nchi hiyo inazidi kupanua mradi wake wa kinuklea na kukorofisha shughuli za shirika hilo la Umoja wa mataifa.
Ripoti hiyo inashadidia lawama zilizotolewa na katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon kuhusu mipango ya kinuklia ya Iran,katika mkutano huo wa siku mbili uliopangwa kumalizika hii leo.
Katika hotuba yake ya ufunguzi kiongozi mkuu wa Iran,Ayatollah Ali Khamenei alizishambulia Marekani,Israel na baraza la Usalama la Umoja wa mataifa anazozituhumu kuwa msatari wa mbele katika shinikizo la kimataifa dhidi ya nchi yake.
Alisema nchi yake haitasitisha harakati zake za kinuklea,licha ya vikwazo vya Umoja wa mataifa na nchi za magharibi na kusisitiza mradai wao haujalenga kutengeneza silaha za kinuklea ambazo matumizi yake yake anayalinganisha na "dhambi lisilosameheka."
Ripoti ya shirika la kimataifa la nguvu za atomiki,iliyochapishwa jana usiku,mnamo kilele cha mkutano wa kilele wa jumuia ya nchi zisizofungamana na upande wowote mjini Teheran,inasema Iran imezidisha maradufu uwezo wake wa kurutubisha maadini ya Uranium katika vituo vyake vya chini kwa chini-lakini bado haijafungulia mitambo yake zaidi ya elfu moja .
Ripoti hiyo imesema pia kwamba wachunguzi wa Umoja wa mataifa waliotaka kukitembelea kituo cha kijeshi cha Parchin,nje ya mji mkuu Teheran-wamekuwa wakikataliwa ruhusa tangu miezi kadhaa sasa.Inadhaniwa kwamba majaribio ya kuripua vichwa vya kinuklea yamekuwa yakifanyika katika kituo hicho ambacho kimefunikwa kwa namna ambayo hakiwezi kunaswa na satelite.
Mwanaachama mmoja wa tume ya bunge la Iran inayosahughulikia masuala ya usalama wa taifa na siasa ya nje,Hossein Naqafi amenukuliwa na shirika la habari la Iran -ISNA akisema wakati wa kuchapioshwa ripoti hiyo umechaguliwa makusudi kwa lengo la kudhoofisha mkutano wa kilele wa jumuiya ya nchi zisizofungamana na upande wowote.
"Hakuna kipya katika ripoti hiyo,inazungumzia madai yale yale ya zamani ya shirika hilo" amesema mbunge huyo .
Ikulu ya Marekani imesema daima serikali ya Marekani imekuwa ikiitanabahisha Iran imesaaliwa na muda mchache tu kusitisha harakatai zake za kinuklea na kwamba mapendekezo ya nchi za magharibi hayatasalia milele katika meza ya majadiliano.
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa,Ban Ki-Moon,akiwa katika ziara yake ya kwanza nchini Iran wiki hii,aliwaambia Khamenei na rais Mahmoud Ahmadinedjad nchi yao inabidi ichukue hatua thabiti kuondowa wasi wasi wa walimwengu na kujiambatanisha na maazimio ya shirika la kimataifa la nguvu za Atomiki na yale ya Umoja wa mataifa.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman