Ripoti ya UN: Vina vya bahari duniani vyapanda maradufu
21 Aprili 2023Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa limesema vina vya bahari duniani kote vinaendelea kupanda kwa kasi ya kuliko kasi ya viwango vilivyopimwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 1993 hadi 2002. Shirika hilo limesema viwango vya sasa vimegonga kima cha juu.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa katika ripoti yake inayoelezea maafa yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa limesema barafu iliyokithiri iliyeyuka pamoja na kuongezeka viwango vya joto baharini ambavyo vilisababisha maji kujaa na kuchangia kasi ya kupanda kina cha maji ya bahari kufikia milimita 4.62 kati ya mwaka 2013 na 2022. Kiwango hicho ni ongezeko maradufu katika kipindi cha mwaka 1993 hadi 2002 ambapo hali hiyo ilisababisha ongezeko la jumla la zaidi ya centimita10 tangu mwanzoni mwa miaka ya 90.
Katibu Mkuu wa Shrika la Umoja wa Mataifa la hali ya Hewa (WMO) Petteri Taalas, amesema kuongezeka kwa vina vya maji baharini kunatishia baadhi ya miji ya pwani hasa ile iliyo kwenye nyada za chini kama kisiwa cha Tuvalu kilicho katikati ya Hawaii na Australia kwenye bahari ya Pasifiki kusini ambacho kufikia sasa kinapanga kujijengea mifumo ya kidijitali itakayowasaidia watu wa kisiwa hicho iwapo kitakumbwa na mafuriko.
Ripoti hiyo inaonesha kwamba, gesi chafu na viwango vya mabaki ya gesi chafu hewani vinaendelea kupanda kwa kasi hali inayochangia ongezeko la joto kwenye ardhi, baharini na kuyeyuka kwa barafu vinavyosababisha vina vya bahari kupanda na pia kusababisha ongezeko la joto na tindikali baharini.
Kwa jumla ripoti hiyo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani imeserma miaka minane iliyopita imekuwa ya joto kali zaidi kuwahi kuorodheshwa huku viwango vya gesi chafu kama hewa ya ukaa vikifikia kilele kipya.
Katibu Mkuu wa Shrika la Umoja wa Mataifa la hali ya Hewa (WMO) Petteri Taalas amesema licha ya habari mbaya kwenye ripoti hiyo lakini kuna kila sababu ya kuwa na matumaini kwa sababu tunaweza kujiondoa kutoka kwenye hali hii mbaya na kuyafikia malengo ya kiwango cha digrii 1.5 kwa kuzingatia mipango kabambe ya hali ya hewa kutoka kwa nchi za G7 ambazo amesema zinaweza kuuwezesha ulimwengu kufikia malengo ya mkataba wa Paris wa mwaka 2015.
Chanzo:/RTRE