1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya Marekani: Uturuki imepeleka wapiganaji Libya

Sekione Kitojo
18 Julai 2020

 Kwa mujibu wa ripoti mpya ya  wizara ya ulinzi ya Marekani, Uturuki imepeleka  kati ya  wapiganaji 3,500 na  3,800  nchini  Libya katika kipindi cha  miezi mitatu ya  mwaka  huu.

Libyen Truppen von General Haftar zurückgedrängt
Wapiganaji watiifu kwa serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa mjini Tripoli wakishangilia ushindi dhidi ya majeshi ya HaftarPicha: Getty Images/AFP/M. Turkia

Ripoti hiyo ni  ya  kwanza  kutoa  maelezo  ya jinsi Uturuki inavyopeleka  wapiganaji  ambao  wanajaribu  kusaidia  kubadilisha mkondo  wa  vita  nchini  Libya.

Hulusi Akar waziri wa ulinzi wa Uturuki akiwa na wanajeshi wa Uturuki nchini LibyaPicha: DHA

Ripoti hiyo inakuja  wakati mzozo  katika  nchi  hiyo  yenye  utajiri mkubwa  wa  mafuta unaongezeka  na  kuwa  vita vya mataifa  ya kigeni yanayopigana  ndani ya nchi  hiyo vita vinavyochochewa  na mataifa  hayo ya kigeni  kwa  kuingiza  silaha na  wapiganaji mamluki  nchini Libya.

Jeshi  la  Marekani  limekuwa  na  wasi  wsi  mkubwa  juu ya ushawishi  wa Urusi  nchini  Libya, ambako  mamia  ya  wapiganaji mamluki  wa  Urusi  wanaunga  mkono  kampeni ya  kuukamata  mji mkuu , Tripoli, upande  wa  magharibi  ya  nchi  hiyo.

Ripoti  hiyo  ya  robo  mwaka kuhusu operesheni za  kupambana  na ugaidi  katika  bara  la  Afrika  iliyotolewa  na  kitengo cha uangalizi cha  wizara ya ulinzi, na  kuchapishwa  siku  ya  Alhamis, imesema Uturuki  imelipa na  kutoa  uraia kwa  maelfu ya  wapiganaji  mamluki wanaopigana  pamoja  na  wanamgambo  wenye  makao  yao  mjini Tripoli dhidi  ya  vikosi vya  kamanda  aliyeko  upande  wa  mashariki nchini  Libya  Khalifa Haftar.

Mpiganaji wa jeshi tiifu la serikali inayotambuliwa kimataifa akionyesha alama ya ushindiPicha: Getty Images/AFP/M. Turkia

Mafungamano na  al-Qaeda

Licha  ya  ripoti zilizozagaa  za  mahusiano  na  wapiganaji  wenye itikadi  kali, ripoti  hiyo inasema  jeshi  la  Marekani  halikupata ushahidi  kuonesha  kwamba  wapiganaji  hao  mamluki  wana mafungamano na  kundi  la  itikadi  kali   linalojiita  Dola  la  Kiislamu ama  al-Qaida. Imesema ripoti  hiyo kwamba  kuna  uwezekano mkubwa  kuwa  walihamasishwa  na  kiasi  kikubwa cha  fedha badala  ya  nadharia ama siasa.

Ripoti  hiyo  inajumuisha tu robo  ya  kwanza  ya  mwaka, hadi mwisho  wa  mwezi  Machi, miezi  miwili  kabla  ya mfululizo  wa ushindi uliopata  usaidizi  kutoka  Uturuki wa  majeshi  ya serikali  ya Tripoli  na  kuyafurusha  majeshi ya  Haftar kutoka  katika  maeneo ya  karibu  na  mji  huo  mkuu, katika  ngome  yake  kuu  ya  Tarhuna na  kituo kikuu cha  jeshi  la  anga  upande wa  magharibi.

Kubadilishwa  kwa  mafanikio ya  Haftar  na  waungaji  wake  mkono wa kigeni, ikiwa ni pamoja  na  Misri, Urusi na  Umoja  wa  Falme  za kiarabu, kumemulika  uhusika  unaoongezeka wa  Uturuki katika vita hivyo  vya  mataifa  ya  nje  ndani  ya  Libya.

Khalifa Haftar kamanda wa majeshi ya upande wa mashariki mwa LibyaPicha: Getty Images/S. Gallup

Ripoti  hiyo ya  hivi  karibuni  inasema  upelekaji  wa  majeshi unaofanywa  na  Uturuki  huenda  uliongezeka  kabla  ya  ushindi  wa majeshi  ya  serikali  ya  Tripoli mwishoni  mwa  mwezi  Mei.

Inanukuu  kamandi ya  majeshi  ya  Marekani  katika  Afrika  ikisema kuwa waasi 300  wa  Syria  waliokuwa  wakisaidiwa  na  Uturuki waliwasili  nchini  Libya mapema  mwezi  Aprili. Uturuki  pia  iliweka "idadi  isiyojulikana" ya  wanajeshi  wa  Uturuki katika  miezi  ya mwanzo  ya  mwaka  huu, mrakibu  mkuu  aliongeza.