1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yalaumiwa kwa vitendo vya ubaguzi wa rangi

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
1 Februari 2022

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limechapisha ripoti yake inayo itaja Israel kuwa ni taifa linalozingatia ubaguzi wa rangi na linalowachukulia Wapalestina kama kundi la watu duni.

Jahresbericht von Amnesty International
Picha: Monika Skolimowska/dpa/picture alliance

Amnesty International imeungana na mashirika mengine ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu ambayo Israel inayapinga na inasema haitambui madai ya mashirika hayo. Mashirika hayo ya kutetea haki za binadamu ni pamoja na shirika la nchini Israel linaloitwa B'Tselem ambalo mwaka mmoja uliopita liliingia katika lawama baada ya kusema kwamba sera za Israel zilielekezwa katika kuzikalia sehemu za mto Jordan hadi bahari ya Mediterania na hivyo kufananishwa na utawala wa kibaguzi wa makaburu. B'Tselem pia inailaumu Israel kwa kutenda uhalifu wa ubaguzi kutokana na historia ya miaka takriban 55 ya kuzikalia sehemu za wapalestina ambazo wanazihitaji kwa ajili ya nchi yao ya baadae. Wameilaumu Israel jinsi inavyowatendea waarabu ambao ni jamii ya wachache.

Mwanajeshi wa Israel akiwa katika ulinzi katika kizuizi kipya cha chini ya ardhi kilichokamilika kwenye mpaka wa Israel na Ukanda wa Gaza. Israel ilitangaza kukamilika kwa kizuizi hicho tarehe 07.12.2021.Picha: Tsafrir Abayov/AP/picture alliance

Shirika jingine la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lenye makao yake makuu nchini Marekani ndio la kwanza kutoa hadharani madai dhidi ya Israel. Kwa upande wake shirika la Amnesty International limeeleza kuwa sera za Israel zinatimiza vigezo vya sera za kibaguzi za utawala wa makaburu kulingana na jinsi inavyofafanuliwa katika sheria za kimataifa.

Katibu mkuu wa shirika la Amnesty International Agnes Callamard amesema ripoti iliyotolewa na asasi yake imo katika msingi wa miito ya hapo awali inayodai kwamba sera za kibaguzi zinatekelezwa katika maeneo ya wapalestina yanayokaliwa na Israel, ambamo idadi ya raia wa kiarabu inavuka asilimia 20.

Callamard amesema Wapalestina wanachukuliwa kama binadamu wa daraja la chini iwe kwenye ukingo wa magharibi, Ukanda wa Gaza ama Jerusalem Mashariki. Amesema Wapalestina wananyimwa haki zao. Ameeleza kuwa sera za Israel kwenye maeneo ya wapalestina yanayokaliwa ni za kibaguzi.

Katibu mkuu wa shirika la Amnesty International Agnes Callamard Picha: Claudio Bresciani/TT News Agency/picture alliance

Israel hapo jana Jumatatu ilitoa wito kwa shirika la Amnesty International kutochapisha ripoti hiyo inayoishutumu nchi hiyo kwa ubaguzi wa rangi, ikisema madai ya shirika hilo la kimataifa la haki za binadamu lenye makao yake mjini London, Uingereza ni ya uongo, upendeleo na chuki dhidi ya Wayahudi. Katibu mkuu wa Amnesty International Agnes Callamard, akizungumzua juu ya ripoti ya shirika lake amesema ripoti hiyo imezingatia sheria, sera na utendaji wa taifa la Israel dhidi ya watu wa Palestina. Na wala sio chuki dhidi ya Wayahudi, Ripoti hii ni kinyume chake kwani inaangazia ukiukwaji unaofanywa dhidi ya watu ambao ni sehemu ya taifa la Israeli.

Soma zaidi: Wapalestina waukataa uamuzi wa Mahakama ya Israel

Ripoti ya kurasa 278 ya Shirikal la Amnesty International ilikusanywa kwa kipindi cha miaka minne na shirika hilo limesema matokeo ya ripoti hiyo ni sehemu ya harakati za kimataifa zinazoongezeka kutaka upatikane ufumbuzi mpya wa mzozo wa Israel na Palestina kwa kusisitiza usawa kwa pande zote badala ya mzozo huo kuangaliwa kuwa ni mzozo wa kikanda.

Juhudi hizo zimepata nguvu katika kipindi cha muongo mmoja tangu mchakato wa amani ulipositishwa huku Israel ikiendelea kuiimarisha udhibiti wake wa maeneo inayokalia kimabavu na kuendelea kulivuruga wazo la kuzaliwa taifa huru la Palestina.

Vyanzo: AP/AFP/RTRE

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW