1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

FAO: Njaa duniani sababu ni uhaba na bei za juu za vyakula

24 Januari 2023

Ripoti mpya ya Shirika la Kilimo na Chakula, FAO pamoja na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa imesema idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba wa chakula barani Asia inaongezeka.

Mario Lubetkin, von FAO-Regionalbeauftragter für Lateinamerika und die Karibik
Picha: Max Valencia/FAO

Ripoti hiyo ya kila mwaka ni ya tano inayoandaliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiwemo shirika la kilimo na chakula FAO, shirika la linaloshughulikia maswala ya Watoto, UNICEF, shirika la Afya Duniani, WHO na shirika la mpango wa chakula duniani, WFP kuhusu uhaba wa chakula na hatari ya kuzuka baa la njaa kwenye maeneo mbalimbali duniani.

Josette Sheeran, Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).Picha: dapd

Mashirika hayo yamesema katika ripoti hiyo kwamba takriban watu nusu bilioni au watu wanane kati ya watu 10 walipata lishe duni katika eneo la Asia Kusini mnamo mwaka 2021 na zaidi ya watu bilioni 1 walikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Ulimwenguni kote uhaba wa chakula iliongezeka hadi asilimia 29 katika mwaka huo wa 2021 kutoka asilimia 21 tangu mwaka 2014.

Ripoti hiyo imelitaja janga la COVID-19 kuwa kikwazo kikubwa, na ambalo lilisababisha kiwango kikubwa cha watu kupoteza ajira. Vilevile imegusia vita vya nchini Ukraine kuwa pia ni sababu ya kuongezeka kwa bei za chakula, nishati na mbolea, hali inayowatumbukiza mamilioni ya watu katika adha ya kukosa fursa za kujitafutia mlo wa kutosha.

Mashirika hayo yamesema katika miaka hiyo juhudi za kupunguza njaa na matatizo ya utapiamlokutokana na lishe duni zimekwama. Pia imeangazia ukosefu wa uhakika wa kupata chakula unaowakabili watu waliohamia mijini, ambapo ni vigumu kwao kupata chakula cha bei nafuu.

Mashirika hayo ya Umoja wa mataifa yamesema ni muhimu kufanyike marekebisho katika mifumo ya kilimo ili kuwezesha uzalishaji wa chakula chenye lishe bora na wakati huo huo kuhakikisha upatikanaji wa lishe bora kwa wote.

Faharasi ya bei ya vyakula ya shirika la FAO imeonesha kupanda sana kwa bei za vyakula katika miaka kadhaa iliyopita, ambapo mwezi Machi mwaka uliopita wa 2022 ukiorodheshwa kuwa ni wakati ambapo bei za vyakula zilipanda mno.

Sudan: Mkulima anavuna mtama unaozalishwa kutokana na mbegu zilizotolewa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO)Picha: CC/United Nation Photos

Eneo la Asia ya Pasifiki huagiza chakula kwa gharama za karibu dola trilioni 2 kwa mwaka. Na hivyo kupanda kwa bei za vyakula vya msingi kama  mchele, ngano na mafuta ya kupikia ni pigo kubwa kwa jamii masikini na kuongeza hali ngumu kwa jamii hizo.

Soma:Bei ya chakula duniani ilifikia rekodi ya juu mwaka 2022

Mwandishi wa ripoti hiyo wa shirika la FAO, Sridhar Dharmapuri, katika kuielezea hali hiyo mbaya amesema kuongezeka kwa umasikini kunaenda sambamba na uhaba wa chakula, mambo yatakayohatarisha hali ya afya na tija ya jamii katika siku za usoni kwani hali hiyo itasababisha watoto kukumbwa na maradhi ya udumavu na pia kuwafanya wawe rahisi kushambuliwa na magonjwa mengine. Karibu robo ya watoto kwenye bara la  Asia-Pasifiki tayari wameathiriwa na udumavu au wana urefu mdogo kulingana na umri wao amesema Dharmapuri katika maelezo yake kwenye ripoti hiyo.

Chanzo:AP