Ripoti ya SIPRI- matumizi ya kijeshi yaongezeka duniani
29 Aprili 2019Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa amani mjini Stockholm (SIPRI) imekadiria kwamba matumizi ya dunia ya kijeshi yamefikia jumla ya dola za Marekani trilioni 1.8 katika mwaka 2018, ikiwa ni juu kwa asilimia 2.6 kutoka mwaka 2017.
Idadi hiyo inatafsirika kuwa ni sawa na dola 239 kwa mtu mmoja, kwa mujibu wa SIPRI. Marekani imebakia kuwa nchi ya kwanza duniani kwa matumizi makubwa ya kijeshi kwa kutumia dola bilioni 649, ikiwa ni ongezeko kutoka mwaka mmoja uliopita la asilimia 4.
„Ongezeko hilo katika matumizi ya Marekani limesababishwa na utekelezaji kutoka mwaka 2017 wa mipango mipya ya ununuzi wa silaha chini ya utawala wa rais wa Marekani Donald Trump," amesema Aude Fleurant , mkurugenzi wa mpango wa SIPRI wa matumizi ya jeshi na ununuzi wa silaha.
Marekani imechangia jumla ya asilimia 36 ya matumizi yote ya dunia katika mwaka 2018, na ilitumia karibu kiasi kama hicho kwa jumla ya mataifa mengine manane yaliyofanya manunuzi ya juu, SIPRI imesema. Hata hivyo, matumizi ya Marekani yalikuwa karibu moja ya tano chini kuliko matumizi yake ya juu kabisa mwaka 2010.
Matumizi ya nchi iliyoshika nafasi ya pili China yalikadiriwa kuwa dola bilioni 250, ikiwa sawa na asilimia 14 ya matumizi yote ya dunia.
Matumizi hayo yalikuwa yameongezeka kwa asilimia 5 katika mwaka 2018, ikiwakilisha ongezeko la chini la China kwa mwaka tangu mwaka 1996 na linaakisi ukuaji wa taratibu wa uchumi.
„Ongezeko la matumizi ya kijeshi kwa China linafuata ukuaji jumla wa uchumi wa nchi hiyo," mtafiti wa SIPRI Nan Tian amesema.
Saudi Arabia imebaki katika nafasi ya tatu kwa kutumia dola bilioni 67.6, licha ya kupunguza matumizi ya asilimia 6 ikilinganishwa na mwaka 2017, ikifuatiwa na India na Ufaransa. Akizungumza na DW mkuu huyo wa kitengo cha utafiti katika SIPRI Nan Tian alisema hata hivyo kuwa matumizi haya sio mashindano ya silaha:
O-Ton Nan Tian:
"Siwezi kusema ni mashindano ya silaha, lakini nchi hizi bila shaka zinaendelea kujihami kwa silaha mpya na zilizobora zaidi na zenye uwezo mzuri zaidi. Na silaha hizi mara nyingi ni ghali sana."
Matumizi ya India yameongezeka kwa mwaka wa tano mfululizo, kwa kiasi hali hiyo kikubwa ikisababishwa na hali ya wasi wasi na China na Pakistan, kwa mujibu wa taasisi hiyo. Mataifa matano ya juu watumiaji wakuu yamechangia asilimia 60 ya matumizi yote kijeshi duniani.
Urusi imeporomoka hadi katika nafasi ya sita, ikitumia kiasi kinachokadiriwa kufikia dola bilioni 61.4. Hii ni mara ya kwanza kwa Urusi kutokuwa miongoni mwa nchi tano za juu zenye matumizi makubwa tangu mwaka 2006. SIPRI imeongeza kuwa matumizi ya Urusi bado yalikuwa juu kwa robo ikilinganishwa na mwaka 2009.
Mataifa 10 ya juu yaliyotumia fedha nyingi kwa ajili ya jeshi ni pamoja na Uingereza, Ujerumani, Japan na Korea kusini.
Kwa utaratibu wa jumla kwa mujibu wa SIPRI ni kwamba matumizi kwa ajili ya jeshi kama sehemu ya pato jumla la taifa yamepungua katika kanda zote tangu mwaka 1999.
SIPRI imesema kwamba sita kati ya mataifa 10 ambayo matumizi ya jeshi yanakadiriwa kuchukua sehemu kubwa ya pato jumla la taifa GDP,ambayo pia yanaelezwa kuwa jeshi ni mzigo, yanapatikana katika mashariki ya kati.
Mataifa hayo ni pamoja na Saudi Arabia katika asilimia 8.8, Oman katika asilimia 8.2, na Israel katika asilimia 4.3.
SIPRI imesema kinashindwa kupata data kutoka mataifa kadhaa ikiwa ni pamoja na Syria, Umoja wa falme za Kiarabu, Qatar na Yemen. Lakini kwa mujibu wa data zilizopo , mzigo wa jeshi katika mashariki ya kati ni asilimia 4.4 ya pato jumla la taifa. Barani Ulaya mzigo wa jeshi uko katika wastani wa asilimia 1.6, kiasi kidogo chini ya Afrika na maeneo ya Asia na mataifa ya bahari ya Pacifiki.