Ripoti ya taasisi ya SIPRIS kuhusu biashara ya silaha
12 Machi 2018Tunaanzia Stockholm ilikochapishwa ripoti ya taasisi ya kimataifa inayochunguza masuala ya amani Sipri. Taasisi hiyo inasema biashara ya silaha imeongezeka kupita kiasi. Gazeti la "Volksstimme" linaandika. "Taasisi hiyo ya Sipri inatathmini na kulinganisha biashara ya silaha ulimwenguni. Kwa mujibu wa tathmini hizo,Ujerumani inaendelea tangu miaka mitano iliyopita kudhibiti nafasi ya nne kama muuzaji mkubwa wa silaha ulimwenguni. Biashara jumla ya silaha za Ujerumani imepungua lakini kwa kipindi hicho hicho kwa asili mia 14, ingawa silaha ilizouza katika maeneo ya mizozo Mashariki ya kati imeongezeka mara dufu kati ya mwaka 2008 hadi 2012. Wakati huo China imeongeza kwa asili mia 34 biashara yake ya silaha huku biashara ya silaha ya Marekani ikiongezeka kwa asili mia 25. Hoja kwamba baadhi ya nchi zimeuza kidogo na nyengine zimeuza nyingi haina uzito wowote upande huo. Mahitaji yanapojitokeza kokote kule, nchi nyengine inapeleka. Ukweli kwamba kuwepo silaha ndiko kunakorahisha mizozo ya mtutu wa bunduki, haujaanza leo kujulikana. Na kinyume chake pia ndio hivyo hivyo, uhaba wa biashara ya silaha haimaanishi kuwa sababu ya amani duniani. Na kwa wakati wote ambao mbio za kutengeneza silaha zitaleta faida nono, hakuna kitakachobadilika."
Trump atishia kuzusha vita vya kibiashara
Rais wa Marekani Donald Trump anaendelea na sera zake za kutanguliza mbele masilahi ya Marekani, au "America First" kama mwenyewe anavyosema. Gazeti la "Neue Westfälisches" linamulika kitisho cha vita vya kibiashara na kuandika: "Eti mara ngapi Donald Trump ameonekana hafai? Si kweli hata kidogo, tajiri huyo mkubwa mwenye kumiliki majumba ana nguvu za kutosha kuvunja sheria zilizoko na kulazimisha zake zifuatwe. Wote wale watakaokwepa kufuata amri yake anawatisha kwa vita vya kibiashara. Na hakuna shaka nchi yake itamfuata ikilazimika. Kimsingi kutokana na matamshi yake ya kibaguzi na pia matusi, thuluthi mbili ya wamarekani wangebidi kumgeukia; lakini hali ni nyengine kabisa na yadhihirikia sera zake zimeanza kuleta tija."
Xi ajiandaa kutawala hadi mwisho wa maisha yake
Mada yetu ya mwisho magazetini inatufikisha jamhuri ya umma wa China ambako wawakilishi zaidi ya elfu tatu wa nchi hiyo wamepiga kura kuondoa kikomo cha mhula, uamuzi utakaomfungulia njia rais Xi Jinping kutawala hadi mwisho wa maisha yake. Gazeti la "Landeszeitung" linaandika: "Uamuzi huo ni pigo kwa nchi za magharibi na kitisho pia. Pigo kwasababu nchi za magharibi daima zimekuwa zikiamini soko huru ndio mlango wa kuelekea uhuru mkubwa zaidi, na uwazi, kwa ufupi demokrasia. Kutokana na siasa ya ubepari China iko njiani kuipita Ulaya kama nguvu ya kiuchumi, lakini katika suala la haki za binaadam, China bado iko nyuma. Kitisho kikubwa kinakutikana ndani ya nchi hiyo kwasababu kinatishia kuenea pia nje ya mipaka ya nchi hiyo."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman