Ripoti ya Umoja wa Mataifa juu ya Mauaji ya Bhutto.
16 Aprili 2010Matangazo
Ripoti hiyo iliyoandaliwa na jopo la watu watatu wakiongozwa na Balozi wa Chile katika Umoja wa Mataifa Heraldo Munoz, iliwasilishwa jana kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon. Ripoti imesema kwamba mauaji ya bibi Bhutto yangeweza kuzuilika iwapo hatua za kutosha za kiusalama zingechukuliwa na kwamba jopo hilo lililokuwa na kazi ya kuweka wazi jambo ambalo lilitendeka na mazingira ya mauaji hayo, limesema linaamini kwamba kushindwa kwa polisi wa Pakistan kuchunguza mauaji hayo ipasavyo kulikwa ni kile walichokiita makusudi au kwa kudhamiria, kutokana na maafisa hao wa polisi kwa kiasi fulani kuogopa kujihusisha kwa mashirika ya kijasusi, katika uchunguzi huo. Aidha ripoti hiyo pia imesema uchunguzi huo uliofanywa na tume hiyo ya Umoja wa mataifa ulikuwa ukizuiwa vikali na mashirika ya kipelelezi pamoja na maafisa wengine ambao walikuwa wakikwamisha kutafutwa kwa ''ukweli ulio huru.'' Ripoti hiyo pia imeeleza kwamba Rais wa wakati huo Pervez Musharaff alikuwa akitambua vitisho vinavyomkabili bibi Bhutto lakini serikali yake hauchukua hatua zozote madhubuti, huku ikieleza kubaguliwa kwa Bibi Bhutto tofauti na mawaziri wengine wakuu wastaafu ambao walikuwa wakipewa ulinzi mkubwa. Benazir Bhutto, mwanamke wa kwanza kuwa Waziri Mkuu nchini Pakistan aliuawa Desemba 27, mwaka 2007, katika shambulio la kujitoa mhanga, baada ya kuhutubia mkutano katika kampeni za uchaguzi mjini Rawalpindi, mji ambao uko karibu na mji mkuu wa nchi hiyo Islamabad. Kifo chake hicho kilisababisha ghasia katika taifa hilo pekee la kiislamu linalomiliki silaha za nyuklia, na kwamba ghasia hizo zilimalizika baada ya mumwe bibi Bhutto Asif Ali Zardari kushinda uchaguzi wa raia nchini humo. Ripoti hiyo lakini haikumtaja mtu wanaeamini kuhusika na mauaji hayo , lakini imependekeza kuwa uchunguzi wowote utakaostahili kufanywa, lazima uangalie wale wote waliohusika kufikiria, kupanga na kufadhili operesheni hiyo na pia wasiache kuondoa uwezekano wa kuhusika kwa jeshi la pakistan. Ripoti hiyo ilifanikishwa baada ya kuhoji watu zaidi ya 250, kukutana na maafisa wa serikali, raia wa kawaida, raia wa kigeni wenye kuyaelewa matukio hayo pamoja na wachunguzi wa kitengo cha kupambana na ugaidi kutoka katika jeshi la polisi la Uingereza -Scotland Yard- ambao walisaidia kuchunguza mauaji hayo. Hata hivyo kiongozi wa jopo hilo la uchunguzi la umoja wa mataifa balozi Heraldo Munoz kutoka Chile amewaambia waandishi wa habari kwamba , uchunguzi huo walioufanya, ulioanza Julai mwaka jana haukuwa uchunguzi wa makosa ya jinai. Wakati huo huo serikali ya Pakistan imesema itatoa kauli yake juu ya ripoti hiyo iliyoandaliwa na jopo lililoteuliwa na Umoja wa Mataifa baada ya kumaliza kuisoma. Mwandishi: Halima Nyanza(afp,Reuters) Mhariri: Sekione Kitojo.
Matangazo