1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RIPOTI YA UNICEF JUU YA ULEZI WA WATOTO

15 Februari 2007

Ripoti ya shirika la UM linalowahudumia watoto linaituhumu hasa uingereza na Marekani miongoni mwa dola za viwanda kupuuza mno kuwashughulikia watoto.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia watoto ulimwenguni-UNICEF- limezilaani Uingereza na Marekani, kuwa ni nchi mbaya kabisa za kuwalea na kuwakuza watoto miongoni mwa nchi tajiri ulimwenguni.Hii inatokana na ripoti iliochapishwa jana mjini Geneva.

Holland,Sweden,Denmark na Finland ndizo zilizo usoni kabisa miongoni mwa nchi 21 za kiviwanda zilizotathminiwa kushughulikia maisha bora kwa watoto.

Watoto waishio Uingereza ndio wenye taabu kabisa na matatizo na wazee wao na wanaowatunza na ndio wanaoathirika zaidi na umasikini na kuangukia zaidi ulevi wa pombe.

Marekani imeangukia nafasi ya 20 na Uingereza ya mwisho ya 21 katika orodha hiyo.Ikistushwa na nafasi hiyo, katika orodha hii iliochapishwa katika ukurasa wa usoni wa kila gazeti huko Uingereza ,serikali ya uingereza iridai taarifa nyingi zilizotumiwa kutunga ripoti hii ni za zamani .

Lakini kikundi kinachotetea haki za watoto kimeonya huko Uingereza kwamba kuna msukosuko katika kitovu cha jamii ya Uingereza.Kimesema na ninanukulu, “Licha ya kuwa nchi tapiri,Uingereza haiwatazami ipasavyo wanawe katika sehemu nyingi za maisha.” Mwisho wa kunukulu.

Takriban thuluthi moja ya wavulana na wasichana nchini Uingereza katika umri wa miaka 11,13 na 15 wanaripotiwa wamekutikana wamelewa mara 2 au zaidi wakati katika nchi nyengine za kundi la OECD kima ni cha chini ya 15%.Uingereza imepongezwa kwa maendeleo iliopiga katika kuhifadhi usalama wa watoto.

Sweden,Holland na Itali zimefikia pia kiwango sawa na hicho cha maendeleo kwa watoto wao.Si ajabu chini ya hali hii, chama cha upinzani Conservative huko Uingereza kimemtuhumu waziri wa fedha Gordon Brown,anaetarajiwa kumrithi waziri mkuu Tony Blair,amekiendea kinyume kizazi kizima cha watoto wadogo.