Ripoti ya UNICEF: Wanawake na watoto wakimbizi wateseka
28 Februari 2017Bahari ya Mediterania inayozigawanya Libya na Italia imekuwa ndio njia kuu ya watu wanao tafuta hifadhi ya kisiasa na pia kwa wahamiaji wanaotafuta maisha mazuri katika nchi za Ulaya, baada safari kama hizo kudhibitiwa katika bahari ya Uturuki.
Kufikia mwezi Septemba mwaka uliopita walikuwepo wakimbizi robo milioni nchini Libya. wengi wao hadi sasa wanateseka katika maeneo wanakozuiwa. Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limesema katika ripoti yake kwamba sehemu wanazozuiwa watu hao ni sawa na kambi za mateso au jela ziliojengwa kiholela bila kutilia maanani huduma muhimu kama za vyoo.
Ripoti hiyo imeeleza zaidi kuwa makundi yenye kujihami kwa silaha ndiyo yanazisimamia sehemu wanakozuiwa wakimbizi na kutokana na mgogoro wa kisiasa unaoikumba Libya kwa sasa makundi hayo yanaendesha pia kambi zao binafsi huku yakishirikiana na makundi ya wahalifu wenye kuendesha biashara ya kuwasafirisha watu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UNICEF maelfu ya wanawake na watoto wamezuiwa kwa miezi kadhaa katika vituo hivyo vya mateso. Zaidi ya wanawake na watoto 100 waliohojiwa karibu nusu ya idadi hiyo walisema wamebakwa au wamenyanyaswa zaidi ya mara moja. Watoto wengi walisema wanapigwa mara kwa mara huku wasichana wakiwa ndio wanaoteseka zaidi kuliko wavulana.
Mtoto mmoja anayeitwa Jon mwenye umri wa miaka 14 alisema watoto wanateseka kambini humo wanapigwa, wananyimwa chakula na maji. Jon alisafiri peke yake kutoka Nigeria kwa kulikimbia kundi la kigaidi la Boko Haram.
Mkuu wa shirika hilo la watoto la UNICEF Afsan Khan anayeongoza shughuli za wakimbizi katika bara la Ulaya amesema njia hiyo inasimamiwa zaidi na wahalifu wanaosafirisha watu na wale wanao jishughulisha na biashara zingine haramu.
Umoja wa Ulaya unatafuta njia za kuzuia wimbi la wakimbizi kutoka Libya baada ya mwaka jana kulifunga eneo la baharini baina ya Uturuki na Ugiriki lililokuwa likitumiwa na wakimbizi kuingia Ulaya. Mwanzoni mwa mwezi Februari viongozi wa Ulaya waliahidi kuipa Libya fedha na misaada mingine ili kujaribu kupunguza idadi ya wahamiaji wanaosafiri kupitia katika bahari ya Mediterania. Mashirika ya misaada yamelaumu maamuzi hayo ambayo wamesema yatahatarisha zaidi maisha ya wahamiaji walio nchini Libya.
Mwaka jana watu laki moja na elfu themanini na moja waliingia nchini Italia kutokea Libya, zaidi ya watu 4,500 walizama na kati yao walikuwa takriban watoto mia saba.
Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE
Mhariri:Iddi Ssessanga