1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti yaonya kuhusu baa la njaa Gaza

22 Desemba 2023

Ripoti ya taasisi ya kimataifa inayokadiria viwango vya upatikanaji wa chakula – IPC inaonya kuhusu kuzuka kwa baa la njaa katika Ukanda wa Gaza. Wakaazi milioni 2.3 wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula

Gazastreifen Rafah | Lebensmittelverteilung
Ripoti mpya yasema watu milioni 2.3 wanakabiliwa na viwango vya juu vya njaa katika Ukanda wa GazaPicha: Hatem Ali/AP Photo/picture alliance

Kulingana na ripoti hiyo, wakaazi milioni 2.3 wa Ukanda huo kwa sasa wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba mkubwa wa chakula. Ripoti hiyo pia imesema hali hiyo huenda ikawa mbaya zaidi kama mambo yataendelea kusalia kama yalivyo kwa sasa. Shirika hilo la IPC linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa limesema mazingira ya njaa bado hayajashika kasi.

Soma zaidi: Rais wa Misri ajadili na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataaifa juu ya juhudi ya kusimamisha mapigano Gaza

Limetaja kipindi kifupi ambapo watu wamekabiliwa na utapiamlo. Hata hivyo, IPC imeonya kuna uwezekano mkubwa mabadiliko haya yanaweza kutokea kama hali haitaimarika.

Makubaliano ya kusitisha vita Israel-Hamas kurefushwa?

02:12

This browser does not support the video element.

Shirika la kimataifa la kiutu CARE linasema takwimu hizo zinazusha wasiwasi, wakati Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Ujerumani imeyataja makadirio hayo ya IPC kuwa ya kutisha.

Kura ya azimio kuhusu Gaza yaahirishwa tena

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kulipigia kuraleo azimio lililocheleweshwa kwa muda mrefu kuhusu vita vya Israel na Hamas. Hii ni baada ya Marekani kuashiria kuliunga mkono kufuatia upinzani dhidi ya mapendekezo ya rasimu ya awali.

Soma pia: Kura ya Baraza la Usalama kuhusu Gaza yaahirishwa tena

Kura hiyo kwa mara nyingine iliahirishwa jana. Baada ya siku kadhaa za kucheleweshwa, rasimu ya karibuni kabisa iliyoonyeshwa shirika la habari la AFP inatoa wito wa hatua za dharura ili kuruhusu maramoja shughuli za kiutu kwa njia salama, na pia kutengeneza mazingira ya kuwepo mpango endelevu wa usitishwaji wa uhasama.

Hata hivyo haitoi wito wa usitishwaji maramoja wa mapigano. Balozi wa Marekani Linda Thomas-Greenfield aliwaambia waandishi habari jana usiku kuwa kama azimio hilo litawasilishwa kama lilivyo, basi Marekani italiunga mkono. Amekanusha kuwa rasimu ya azimio hilo imedhoofishwa, akisema kuwa bado iko imara na inaliunga mkono kundi la nchi za Kiarabu.

Israel inaendelea kudondosha mabomu katika GazaPicha: Ismael Mohamad/UPI Photo/IMAGO

Mashambulizi yazidi Gaza

Wakati hayo yakijiri, mapigano katika Ukanda wa Gaza yameendelea jana Alhamisi huku Israel ikiendelea kuyapiga maeneo ya ukanda huo huku nalo Kundi la Hamas likidhihirisha uwezo wake wa kufyatua komboa hadi Tel Aviv. Hayo yaliendelea huku pande hizo mbili zikiendelea na mazungumzo magumu ya kutafuta makubaliano mapya ya kusitishwa mapigano. Hamas limeorodheshwa kama kundi la kigaidi na Marekani, Ujerumani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine.

Israel iliyalipua maeneo ya kaskazini wa Gaza kabla ya ndege zake kudondosha mabomu katika maeneo ya kati na kusini.

Hamas walifyatua makombora kuelekea Tel Aviv ambayo yaliharibiwa na mfumo wa ulinzi wa angani wa Israel. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa tena kupambana hadi watakapoliangamiza kundi la Hamas. Nao Hamas wamesema makundi yote ya Kipalestina yamechukua msimamo wa pamoja kuwa hakuna mazungumzo yoyote kuhusu wafungwa au mipango ya kubadilishana wafungwa na mateka, hadi pale mashambulizi ya Israel yatakapositishwa kikamilifu.

Afp, ap, reuters, dpa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW