Ripoti zadai mamia wameuwawa Tanzania kufuatia maandamano
31 Oktoba 2025
Takriban watu 700 wameuawa ndani ya siku tatu kufuatia maandamano ya kupinga uchaguzi nchini Tanzania. Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, Idadi hiyo imetolewa na chama kikuu cha upinzani, CHADEMA.
Hali ya vurugu na mauaji nchini Tanzania imeutia pia wasiwasi Umoja wa Mataifa Geneva, ambao umetowa mwito wa kutaka vikosi vya usalama nchini humo kujizuia kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.
Shirika la habari la AFP limemnukuu Afisa wa ngazi ya juu wa chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA anayeshughulikia masuala ya kigeni, John Kitoka, aliyesema kwamba takriban watu 350 wameuliwa Dar es Salaam na wengine zaidi ya 200 wameuliwa kwenye mji wa mwambao wa ziwa Victoria wa Mwanza.
Lakini pia ameongeza kusema kwamba idadi jumla ya waliouawa ikijumuisha kwenye maeneo mengine imefikia kiasi watu 700 kufuatia vurugu zilizozuka tangu siku ya uchaguzi Jumatano, tarehe 29 Oktoba.
Maandamano yashuhudiwa miji mbali mbali
Miji mbali mbali bado inashuhudia vurugu huku huduma ya mtandao wa Intaneti ikiwa imezimwa nchini humo. Umoja wa Mataifa hivi leo umezungumzia hali inayoendelea nchini Tanzania kwa kutaka uchunguzi ufanyike kuhusu vurugu zinazohusiana na uchaguzi. Seif Magango ambaye ni msemaji wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu amezungumza na waandishi habari.
"Tumeshtushwa na vifo na matukio ya watu kujeruhiwa kutokana na maandamano yanayoendelea yakihusiana na uchaguzi nchini Tanzania. Ripoti za kuaminika tulizozipata zinaonesha kiasi watu 10 wameuawa katika miji yaDar es Salaam, Shinyanga na Morogoro wakati vikosi vya usalama vikitumia bunduki na mabomu ya machozi kutawanya waandamanaji''
Mtafiti wa kikanda wa shirika la Kimataifa kutetea haki za binadamu kuhusu Tanzania na Uganda Roland Ebole amesema washirika wao walioko Tanzania wamesema wameshuhudia maiti kwenye mitaa.
''Wenzetu walioko ndani wametufahamisha kwamba wameshuhudia maiti mitaani. Serikali haina uwazi kuhusiana na suala la idadi ya vifo na wanajaribu kutoa idadi ndogo ya waliokufa lakini wenzetu wanatuambia kwamba huenda ikawa waliouwawa wanakaribia mia moja.''
Waandishi wakigeni wazuia kuripoti uchaguzi
Kwa kiasi kikubwa waandishi habari wa kigeni wakiwa wamezuiwa kuuripoti uchaguzi nchini Tanzania na kufungwa kwa mawasiliano kwa siku ya tatu, imekuwa pia vigumu kupatikana taarifa kutoka ndani.
Lakini chama kikuu cha upinzani Chadema ambacho hakishiriki uchaguzi huu kimesema waandamanaji hivi leo walijitokeza katikati ya mji mkuu wa kibiashara Daresalam na kukabiliwa na polisi wengi pamoja na wanajeshi.
Uchaguzi mkuu nchini Tanzania umetumbukia kwenye machafuko baada ya umma kuingia mitaani kuanzia Daresalam hadi kwenye miji mingine ya taifa hilo, na kuchana picha za rais Samia Suluhu Hassan mgombea wa chama tawala CCM ,kushambulia polisi na vituo vya polisi hali iliyosababisha kuzimwa kwa Internet na kutangazwa amri ya kutotoka nje.
Katika visiwa vya Zanzibar ambako kuna utawala wa ndani mgombea urais wa chama cha Mapinduzi CCM Hussein Ali Mwinyi alitangazwa mshindi jana lakini huko nako chama kikuu cha upinzani ACT Wazalendokimeyakataa matokeo hayo kikisema ni wananchi wamewapoka wananchi sauti yao na suluhisho pekee ni kutoa haki kwa kuitishwa uchaguzi mpya.
Mwenyekiti wa chama hicho na aliyekuwa mgombea urais Othman Masoud Othman, amewaambia wafuasi wake hivi leo kwamba chama chao kitachukuwa uamuzi mwafaka muda sio mrefu.
Wakati ikiwa haijulikani uamuzi huo utakuwa ni upi ni wazi kuwa visiwa hivyo vya bahari ya Hindi vinatumbukia kwa mara nyingine tena kwenye mpasuko mkubwa wa kisiasa ambao imekuwa sehemu ya historia yake tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.