1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Rambirambi zamiminika kutokana na kifo cha Rais wa Iran

20 Mei 2024

Viongozi mbalimbali duniani wameelezea kushtushwa na kihuzunishwa na kifo cha rais wa Iran Ebrahim Raisi, aliyefariki katika ajali ya helikopta pamoja na Waziri wake wa Mambo ya Nje.

Ebrahim Raisi | Mkutano wa 77 wa Baraza  Kuu la UN mjini New York
Rais wa Iran Ebrahim Raisi wakati wa uhai wake alipohutubia kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo September 21, 2022Picha: Timothy A. Clary/AFP/Getty Images

Msiba huo ni mzito na raia wa Iran wamo kwenye majonzi makubwa kutokana na kifo cha rais wao, wanaomboleza huku wakilia kutoka walipopokea tangazo rasmi la kifo cha Rais wao Ebrahim Raisi na Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amirabdollahian ambao ni miongoni mwa maafisa waliopoteza Maisha kwenye ajali ya helikopta katika eneo la milima karibu na Azerbaijan.

Helikopta iliyombeba Rais wa Iran Ibrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian, wajumbe na maafisa kabla ya kupata ajali.Picha: vista.ir

Rambirambi za viongozi mbalimbli duniani

Rais wa Urusi Vladimir Putin katika ujumbe wake amesema Seyed Ebrahim Raisi alikuwa mwanasiasa mahiri ambaye maisha yake yote alijitolea kuitumikia nchi yake.

Amemtaja marehemu rais waIranEbrahim Raisi kama mtu aliyekuwa rafiki wa kweli wa Urusi, na kwamba alitoa mchango mkubwa katika kuuendelzea ujirani mwema na mahusiano kati ya Iran na Urusi hadi kufikia kiwango cha ushirikiano wa kimkakati.

Soma Zaidi:Rais wa Iran aripotiwa kufa katika ajali ya helikopta

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Wang Wenbin amesema katika mkutano na waandishi wa Habari kwamba Rais Xi Jinping amesema "kifo cha kutisha" cha Rais waIran Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta ni hasara kubwa kwa watu wa Iran na kwamba watu wa China wamempoteza rafiki mzuri.

Mabaki ya Helikopta iliyokuwa imembeba marehemu Rais wa Iran Ibrahim Rais na waziri wake wa Mambo ya Nje Hossein Amirabdollahian iliyoangika katika eneo la mlima Varzaghan kaskazini-magharibi mwa IranPicha: Stringer/WANA via REUTERS

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika salamu zake za rambirambi kwa watu wa Iran, serikali na hasa kwa mkuu wa kidini wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ali Khamenei amesema amehuzunishwa sana na kifo cha kiongozi huyo wa Iran akisema Uturuki imo kwenye machungu pamoja na watu wa Iran na anawaombea Mungu awape subira na faraja familia za wafiwa.

Risala za rambirambi zazidi kumiminika 

Waziri Mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohammed Bin Rashid al- Makhtoum amesema "Mioyo yetu iko pamoja nanyi watu wa Iran katika kipindi hiki kigumu".

Rais wa Syria Bashar al- Assad katika salamu zake za rambirambi amethibitisha mshikamano kati ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema atamkumbuka Ebriham Rais jinsi alivyojitolea katika kutekeleza majukumu yake.

Soma Zaidi:Iran yathibitisha kufanya mazungumzo na Marekani nchini Oman  

Rais wa Umoja wa Ulaya Charles Michel amesema jumuiya ya Umoja wa Ulaya inatoa rambirambi zake za dhati kwa watu wa Iran kutokana na kifo cha Rais Ebrahim Raisi na Waziri wake wa Mambo ya Nje Hossein Amirabdollahian,wajumbe wengine na wafanyakazi waliofariki katika ajali ya helikopta. Michel amesema mawazo yao pia wanayaelekeza kwa familia za wahanga wa ajali hiyo mbaya.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni amesema yeye na serikali yake wanashikamana na serikali ya Iran na watu wake katika wakati huu mgumu kufuatia kifo cha Rais wa Iran Ebrahim Raisi.

Timu ya waokoaji iliyofika eneo iliktokea ajali ya helikopta iliyokuwa imembeba rais wa Iran iliyotokea Varzaqan mashariki mwa jimbo la AzerbeijanPicha: Stringer/WANA via REUTERS

Mkuu wa Umoja wa nchi za Kiarabu Ahmed Aboul Gheit, pia ametoa salamu za rambirambi na kuwaombea marehemu wapumzike kwa amani na amewatia moyo wafiwa kwamba wazidishe subira na kumshukuru Mungu.

Salamu zingine za rambimbi zimetolewa na Waziri Mkuu wa Iraq Mohamed Shia al-Sudan ambaye amesema wako pamoja na mkuu wa kidini wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ali Khamenei, serikali na watu wa Iran katika kipindi hiki kigumu.

Soma Zaidi:Marekani yaitaka Iran kutowapa silaha waasi wa Houthi  

Pia Rais wa jimbo la Kurdistan nchini Iraq Nechirvan Barzani, ameserma kifo cha Ebrahim Raisi ni msiba mkubwa, amesema ana imani kwamba watu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wataishinda hasara hii kubwa.

Viongozi wengine waliotoa rambirambi na kuelezea masikitiko yao kutokana na kifo cha rais wa Iran ni pamoja na kiongozi wa kijeshi wa SudanAbdel fatah al- Burhani, Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim, serikali ya Japan kupitia msemaji wake Yoshimasa Hayashi ambapo amesema serikali ya Japan inatoa rambirambi zake kwa serikali na watu wa Iran kutokana na kuondokewa na rais wao na Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo.

Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan Picha: Hannibal Hanschke/AFP/Getty Images

Mfalme Abdullah wa Jordan amesema natoa "Pole zangu nyingi kwa uongozi, serikali na watu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na vifo vya Ndugu zangu Rais Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir Abdullahian, wajumbe na maafisa waliofuatana nao. Mungu awarehemu wote”.

Rais wa Misri Abdel Fatah al Sisi amesema Jumuiya ya nchi za Kiarabu zinasimama pamoja na uongozi wa Iran katika msiba huu mzito.

Soma Zaidi: Iran yasema mazungumzo na mkuu wa IAEA yalikuwa mazuri 

Kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran Ilimesifu mapambano ya mashahidi hao waliokufa kwenye ajali ya helikopta wakati walipokua wanalitumikia taifa lao na kumwomba Mwenyezi Mungu awajaalie rehema zake.

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro amesema Ebrahim Raisi daima ataendelea kuwa binadamu bora, mtetezi wa uhuru wa watu wake na rafiki wa Venezuela bila masharti yoyote.

Salamu za rambirambi pia zimetolewa na rais wa Sri Lanka Ranil Wickremesinghe, amesema amehuzunishwa mno na kifo cha Ebrahim Raisi.

Kundi la Hamas na Mkuu wa Wahouthi nchini Yemen Mohammed Ali al- Houthi pia wamesema wamehuzunishwa na kifo cha rais wa Iran Ebranim Raisi, Waziri wake wa Mambo ya Nje na wote waliokuwemo kwenye helikopta iliyopata ajali.

Vyanzo:RTRE/AFP/DPA