1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rishi Sunak kuwa waziri mkuu mpya wa Uingereza

24 Oktoba 2022

Mwanasiasa wa Uingereza Rishi Sunak amechaguliwa hii leo kuwa kiongozi wa chama chga Conservative na atakuwa waziri mkuu ajaye, baada ya mshindani wake Penny Mordaunt kujitoa katika dakika za mwisho.

Rishi Sunak | ehemaliger britischer Finanzminister
Picha: Aberto Pezzali/AP Photo/picture alliance

Sunak ambaye ni mmoja wa wanasiasa tajiri zaidi nchini Uingereza, na ambaye atakuwa kiongozi wa kwanza wa taifa hilo asiye Mzungu, na muumini wa dini ya Kihindu, ataombwa na Mfalme Charles III kuunda serikali, na kuchukuwa nafasi ya Liz Truss, aliedumu katika nafasi hiyo kwa siku 44 tu kabla ya kujiuzulu.

"Kama afisa wa uchaguzi katika mchakato wa uongozi, naweza kuthibitisha kwamba tumepokea uteuzi halali mmoja tu. Hivyo, Rishi Sunak amechaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha Conservative," alisema Sir Graham Brady, mwenyekiti wa kamati yenye ushawishi ya 1922.

Soma pia: Johnson ajiondoa kinyang'anyiro cha uwaziri mkuu Uingereza

Katika taarifa ya kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho muda mfupi kabla ya kutangazwa mshindi, Penny Modaunt ameutaja ushindi wa Sunak kama uamuzi wa kihistoria, ambao kwa mara nyingine umeonyesha uanuwai na kipaji ndani ya cha chama chao, na kuongeza kuwa anamuunga mkono Rishi kikamilifu.

Ofisi ya waziri mkuu wa Uingereza iliyopo mtaa wa Downing 10.Picha: Daniel Leal/AFP

Mwenyekiti wa chama hicho Jake Berry ametoa wito kwa chama chote kuungana nyuma ya Sunak, wakati akijiandaa kuanza kazi ya kukabiliana na changamoto zilizo mbele yao kama taifa.

Wito wa kuungana nyuma ya Sunak

Berry amesema wakati wa mijadala ya ndani umeisha na kwamba anajua chini ya uongozi wa Rishi Sunak, wanaweza kutekeleza mambo ya kipaumbele kwa watu wa Uingereza.

Sunak mwenye umri wa miaka 42 na waziri wa zamani wa fedha, anakuwa waziri mkuu wa tatu wa Uingereza katika kipindi cha chini ya miezi miwili, akikabiliwa na jukumu la kurejesha utulivu katika taifa linalokabiliana na machafuko ya kisiasa na kiuchumi kwa miaka kadhaa.

Soma pia: Truss ajiuzulu baada ya wiki sita kama waziri mkuu Uingereza

Mtangulizi wake Liz Truss aliangushwa na mpango wake wa kiuchumi uliosababisha mtikisiko katika masoko ya kifedha, kupandisha gharama za maisha kwa wapigakura na kuwakasirisha wengi ndani ya chama chake.

Truss amempongeza Sunak kupitia ukurasa wake wa twitter na kuongeza kuwa anamuunga mkono kikamilifu. Vurugu ndani ya chama cha Conservative zimechochea miito ya uchaguzi mkuu.

Hata hivyo chini ya mfumo wa bunge wa Uingereza, hakuhitaji kuwepo na uchaguzi mpya hadi mwishoni mwa 2024, na Sunak amesema hana mpango wa kuitisha uchaguzi mpya.

Soma pia:Waziri Mkuu Uingereza ahaha kurejesha imani baada ya kuvurunda

Na laiti kama uchaguzi huo ungeitishwa mapema, uchunguzi wa maoni unaonesha hilo lingekuwa janga kwa chama cha Conservative, katika wakati ambapo chama cha upinzani cha Labour kinaongoza kwa tofauti kubwa mno miongoni mwa wapigakura.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW