River Plate mabingwa wa Copa Libertadores
10 Desemba 2018Copa Lebertadores kombe la mabingwa wa mataifa ya America ya kusini sawa na Champions League barani Ulaya ama Champions League barani Afrika mara hii limekwenda kwa River Plate ya Argentina , baada ya mpambano mkali na wa kukata na shoka wa mkondo wa pili jana Jumapili baina ya mahasimu wakubwa wa mji mmoja Buenos Aires , Boca Juniors na River Plate kukipiga hapo jana katika uwanja wa Santiago Beunabeu mjini Madrid. Nyasi ziliwaka moto jana usiku......
Mchezo ulichezwa mjini Madrid lakini sherehe na majonzi yalibakia nchini Argentina. River Plate ilishinda mashindano ya Copa Libertadores kwa kuwashinda mahasimu wao wakubwa Boca Juniors katika fainali ambayo ilidumu kwa mwezi mzima na kuhamishiwa nchini Uhispania kwa mara ya kwanza katika historia kwasabbu ya ghasia za mashabiki kabla ya mchezo wa mkondo wa pili.
Licha ya kuwa uamuzi huo wa shirikisho la kandanda la Argentina kuhamisha mchezo huo uliwakasirisha Wargentina wengi , lakini kila kundi la mashabiki liliiangalia fainali hiyo kwa hamasa, nguvu na hisia na wendawazimu kama ambavyo mchezo huo ungefanyika katika ardhi ya America kusini. mashabiki wa River Plate walimiminika katika eneo la wazi la Obelisk katikati ya jiji la Buenos Aires jana usiku kuishangiria timu yao ikitawazwa mabingwa wa Copa Libertadores.
"Wametuondoa kutoka uwanja wetu, wametuondoa kutoka nchini mwetu, wameleta vurugu kubwa, na tumeshinda pamoja na hayo. Imetosha Boca. Hamna cha kusema. Tumewashinda kila mahali."
Ushindi ni raha sana
Ilikuwa ni furaha kila kona ya jiji la Buenos Aires ambalo lilitekwa na mashibiki wa River Plate
Uwanja huo wa mjini Madrid ambao pia utakuwa mwenyeji wa fainali ya Champions League barani Ulaya mwezi Juni , uliteuliwa kwa sehemu fulani kwasababu ya rekodi yake ya kuwa mwenyeji wa matukio makubwa na usalama, ambao ni pamoja na polisi 2,500 kuwekwa , ili kulinda usalama kabla ya mtanange huo kuanza.
Mashabiki walitenganishwa katika kanda kila upande wa uwanja na walifanyiwa ukaguzi mkali. Vilabu vyote vilipewa tikiti 25,000, na ni 5,000 tu zilizotengwa kwa mashabiki wanaoishi Argentina.
Huyu hapa shabiki wa River Plate Sofia akiwa mjini Buenos Aires akizungumza baada ya mpambano huo.
"Ni furaha kubwa mno, ushindi umeniondolea mzigo baada ya kukosa usingizi kwa wiki kadhaa, kupoteza sauti, na kukosa siku kadhaa za kwenda kazini kwasababu nilikwenda katika michezo miwili ambayo iliahirishwa lakini furaha niliyonayo ni kubwa, na hakuna kinachonipa faraja kubwa kuliko kuvaa jezi hii."
Wakati huo huo baada ya kuiongoza River Plate katika ubingwa wao wa pili wa Copa Libertadores katika misimu minne, kocha Marcelo Gallardo anaonekana kuwa ataelekea katika mataifa ya Ulaya lakini wachezaji wake wana matumaini kwamba uhusiano wake na vigogo hivyo vya soka vya Argentina utamfanya abakie mjini Buenos Aires kwa kipindi kirefu kidogo. Atakwenda Ulaya ktika wakati fulani, lakini kwa sasa yuko nyumbani na ni vigumu kwake kuondoka," nahodha wa River Plate Leonardo Ponzio aliwaambia waandishi habari baada ya ushindi wa River wa mabao 3-1 dhidi ya mahasimu wao Boca Juniors.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / dpae / rtre / afpe
Mhariri: Yusuf Saumu