Riyadh yatoa wito wa mazungumzo kwa makundi hasimu Yemen
3 Januari 2026
Saudi Arabia imetoa wito leo wa mazungumzo kati ya makundi hasmi ya kusini mwa Yemen huku kukiwa na mapigano katika jimbo la Hadramawt lenye utajiri wa rasilimali, ambako Baraza la Mpito la Kusini (STC) linaloungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu lilichukua maeneo makubwa katika wiki za hivi karibuni.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, wizara ya mambo ya nje ya Saudi Arabia imependekeza mkutano kamili huko Riyadh ili kuyakutanisha makundi yote ya kusini ili kujadili suluhisho la haki. Riyadh ilisema mwaliko huo wa mazungumzo umetolewa na serikali ya Yemen.
Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa miaka mingi zimeunga mkono makundi hasimu katika maeneo ya serikali ya Yemen iliyogawika. Wakati huo huo kumeripotiwa milipuko ya risasi mapema leo katika mji mkuu wa jimbo la Hadramawt wa Mukalla.