Marekani: Hakuna ushahidi wa ushirikiano wa Trump na Urusi
25 Machi 2019Kwa mujibu wa muhtasari wa ripoti ya Robert Mueller uliondaliwa na mwanasheria mkuu wa nchini Marekani William Barr, kwenye barua yenye kurasa nne iliyowasilishwa kwa kamati ya wabunge wa Baraza la wawakilishi katika bunge la Marekani, Barr, ameeleza kuwa uchunguzi uliofanywa na Robert Mueller haukuthibitisha iwapo Trump alifanya kosa la jinai.
Mwanasheria mkuu huyo amesema Mueller hakuwa na uhakika kwamba waendesha kampeni ya Trump walipanga au kuhusika na mpango wa serikali ya Urusi wa kuingilia kati ya uchaguzi wa Rais wa Marekani wa mwaka 2016. Akizungumzia juu ya ripoti hiyo Rais Trump amesema hana hatia. Hatua hiyo inampa ushindi mkubwa wa kisiasa Rais Trump.
Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence amesema hitimisho la uchunguzi wa mwanasheria maalum Robert Mueller ni uthibitisho wa jumla kuwa Rais Donald Trump na waendesha kampeni yake wamevuliwa tuhuma mbaya mno na ni muhimu matokeo hayo kupokewa kwa furaha na Wamarekani wanaopenda ukweli na uadilifu uliokuwepo wakati wa uchaguzi. Pence ameiita siku iliyotolewa ripoti hiyo kuwa ni siku muhimu kwa taifa la Marekani, kwa rais Trump na Utawala wake.
Mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje ya Urusi Konstantin Kosachev amesema hatua hiyo inatoa fursa ya kuufufua uhusiano kati ya Marekani na urusi.
Mwanasheria maalum Robert Mueller alitumia karibu miaka miwili kuchunguza madai kwamba Urusi iliingilia kati uchaguzi wa urais wa Marekani na kumsaidia Trump kumshinda mpinzani wake, Hillary Clinton. Lakini pia mwanasheria huyo mkuu amesema uchunguzi huo haujamwondolea Trump madai ya kuzuia sheria kutendeka.
Spika wa bunge Nancy Pelosi na kiongozi wa wa shughuli za bunge Chuck Schumer wote wanachama wa ngazi za juu wa chama cha Democratic wamesema ripoti hiyo inaibua maswali mengi kuliko majibu yaliyopo. Wademocrat wanataka ripoti yote ya mwanasheria maalumu wa Marekani Robert Mueller ichapishwe hadharani.
Vyanzo:p.dw.com/p/3Fb52RTRE/AP