1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Robert Mugabe amefariki dunia

6 Septemba 2019

Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe amefariki wakati akipatiwa matibabu Singapore. Mugabe aliyekuwa na umri wa miaka 95,aliiongoza Zimbabwe kwa takribani miongo minne.

Robert Mugabe
Picha: Getty Images/AFP/P. Magakoe

Kifo chake kinatokea ikiwa ni karibu miaka miwili tangu aondolewe madarakani kwa kile kinachoelezwa kuwa ni mapinduzi ya kijeshi. Rais huyo wa zamani alikuwa akipatiwa matibabu kutokana na ugonjwa ambao haukuwekwa wazi, huko Singapore tangu Aprili mwaka huu.

Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert MugabePicha: Reuters/M. Hutschings

Chanzo cha kifo chake hakijawekwa wazi

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa sababu ya kifo chake msemaji wa hospitali ya Gleneagles ya Singapore, alikataa kusema chochote, kwa sababu ya kuhifadhi faragha ya marehemu. Rais wa sasa wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa alithibitisha kifo cha kiongozi huyo wa zamani wa Zimbabwe katika ukurasa wake wa Twitter.

Akimuelezea kiongozi huyo, Mnangagwa ameandika Mugabe aliekuwa alama ya ukombozi wa Zimbabwe, alitumia muda wa maisha yake wote kuwajengea uwezo watu wake. Na kuongeza kuwa mchango wake katika historia ya taifa hilo na Afrika kwa ujumla hautaweza kusahaulika.

Ishara za awali za ugonjwa wake

Robert Mugabe na aliyekuwa rais wa Iran Mahamoud AhmadinejadPicha: Getty Images/AFP/D. Kwande

Mwezi uliopita Mnangagwa aliliambia taifa la Zimbabwe kwamba Mugabe amelazwa hospitali nje ya taifa hilo na kwamba afya yake ipo katika hatua nzuri. Kwa kawaida katika kipindi chake cha uongozi cha miaka 37 kiongozi huyo wa zamani amekuwa akipatiwa matibabu Singapore na aliendelea na utaratibu huo hata baada ya kuondolewa madarakani kijeshi mwaka 2017 na nafasi yake kuchukuliwa na makamo wake Emmerson Mnangagwa.

Zimbabwe taifa ambalo lilikuwa likijivunia mfumo wake mzuri wa matibabu linaelezwa kuvurugwa na utawala mbovu wa Mugabe na uchumi wake kuporomoka. Hali hiyo ilisababisha wanasiasa wa taifa hilo na raia wenye uwezo kwenda kutafuta matibabu nchini Afrika Kusini na kwengineko katika mataifa ya nje.

Mpigania uhuru huyo wa zamani ambae aliendesha  vita vya msituni dhidi ya utawala wa wazungu wachache katika kipindi ambacho Zimbabwe ikifahamika kama Rhodesia, baadae alipoingia madarakani, akawa mmoja kati ya viongozi wa muda mrefu kabisa barani Afrika.

Bado amekuwa akiheshimiwa na baadhi ya watu barani Afrika kwa vita vyake dhidi ya waliwezi wa kizungu inngawa pia wapo wenye kumtazama kama mtu mwenye kuwajibika moja kwa moja kwa kuuvuruga uchumi wa Zimbabwe na kusababisha vurugu za kuukandamiza upinzani.

Chanzo: dpae

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW