1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Robert Mugabe azikwa

28 Septemba 2019

Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe hatimaye amezikwa kijijini kwake Kutama. Mugabe alifariki wiki tatu zilizopita nchini Singapore alikokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

Simbabwe Beisetzung Robert Mugabe
Picha: Reuters/P. Bulawayo

Mwili wa Mugabe umepumzishwa kwenye ua wa nyumbani kwake katika kijiji cha Kutama, wilaya ya Zvimba kilomita 90 magharibi mwa mji mkuu Harare.

Mamia ya waombolezaji alikusanyika kwenye tukio hilo ambalo awali lilitarajiwa kuwa ni la faragha na kuhusisha familia tu. Wengi wao walikuwa wamevalia fulana nyeupe zilizokuwa na picha ya Mugabe na zilizoandikwa ujumbe "Baba wa taifa", "mkombozi" na "mbeba tochi".

Baadhi yao walikuwa wakiimba na kucheza na wengine walikuwa wamekaa kimya kwenye mahema meupe yaliyoandaliwa maalumu kwa shughuli hiyo. Mkewe Grace Mugabe pamoja na watoto wao walilisindikiza jeneza la Mugabe, lililokuwa limezungushiwa bendera ya Zimbabwe iliyokuwa na rangi ya kijani, njano, nyekundu na nyeusi.

Mke wa Mugabe, Grace Mugabe Picha: Reuters/P. Bulawayo

Padri aliyeongoza ibada ya mazishi alimuomba Mungu amuhurumie Mugabe wakati familia ilipouaga mwili wake na kuongeza kwa kusema kuwa  "mtu huyu ataishi milele".

Hakukua na afisa yoyote mwandamizi wa serikali miongoni mwa waombolezaji.

Familia ya Mugabe iliamua kumzika mwasisi huyo wa taifa katika kijiji cha Kutama baada ya wiki za vuta nikuvute kati ya familia na serikali iliyotaka mwili wake kupumzishwa kwenye makaburi ya kitaifa ya mashujaa mjini Harare. Ulinzi umeimarishwa nchini humo wakati familia hiyo ilipokuwa ikiandaa mazishi yake.

Awali shughuli hiyo ilitarajiwa kuhudhuria na watu waliothibitishwa, tofauti na makubaliano ya awali ya familia na wazee wa kimila kwamba kila mtu angeruhusiwa kuhudhuria.

Msemaji wa chama tawala cha ZANU-PF Simon Khaya Moyo ameyaita mazishi hayo ya faragha kuwa ni hatua ya"kusikitisha sana". 

Mpiganaji huyo wa zamani wa msituni alichukua mamlaka baada ya uhuru kutoka kwa wakoloni mnamo mwaka 1980.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW