1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Robert Zoellick ateuliwa rais mpya wa Benki ya dunia

30 Mei 2007

Rais Gorge W Bush wa Marekani amemteua mwanadiplomasia wa zamani na mkuu wa biashara Robert Zoellick kuwa kiongozi mpya wa benki kuu ya dunia.

Robert Zoellick
Robert ZoellickPicha: AP

Hatua hii inachukuliwa baada kulazimika kujiuzulu kwa Paul Wolfowitz kwenye wadhifa huo kufuatia jinamizi la rushwa lililomuandama kwa muda wa wiki kadhaa.

Kuteuliwa kwa bwana Zoellick ambaye ni mtu shupavu katika masuala nyeti kuanzia biashara ya kimataifa hadi masuala yanayohusu mizozo kama vile Darfur, kunaweza kuonekana kama rais Bush anatafuta hatimaye njia za kuyazima manung'uniko yaliyokuwa yametawala kwenye benki ya dunia katika muda wa wiki kadhaa.

Akizungumza baada ya kuteuliwa kwake bwana Robert Zoellick alisema.

’Ikiwa mtu hana mwelekeo wa mkakati maalum hawezi kukabili Changamoto.’’

Hata hivyo uteuzi huo utabidi kuidhinishwa na bodi ya magavana ya benki ya dunia yenye wanachama 24.

Wolfowitz amekubali kujiuzulu mnamo mwezi juni 30 kumaliza kelele zilizokuwa zinatolewa kufuatia kashfa ya kumpendelea mpenzi wake wa kike ambaye ni mfanyikazi wa benki hiyo kwa kumpandisha cheo na mshahara mnono.

Pamoja na yote lakini uteuzi wa bwana Zoellick huenda ukazusha maswali miongoni mwa nchi za ulaya ambazo zilivunjwa moyo na uteuzi uliofanywa na rais Bush mwaka 2005 wa bwana Wolfowitz, aliyewahi kuwa naibu wa waziri wa ulinzi na vile vile msanifu wa vita vya Iraq.

Bwana Zoellick pia mwenye umri wa miaka 53 aliunga mkono matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya aliyekuwa rais wa Iraq Saddam Hussein.

Zoellick aliwahi kuwa naibu wa waziri wa mambo ya nje Condolezza Rice mwezi Februari mwaka 2005 baada ya kuwa mwakilishi wa Marekani katika masuala ya biashara kwa miaka minne.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu katika utawala war ais Bush anasema uteuzi wa Zoellick unaweza kupokelewa vyema na nchi ambazo zilishauriwa na waziri wa fedha wa Marekani Henry Paulson aliyeongoza harakati za kumtafuta mrithi wa bwana Wolfowitz.

Afisa huyo lakini amekataa kuzitaja nchi hizo.

Afisa huyo ameongeza kusema Robert Zoellick mwenye tajriba ya muda mrefu katika masuala yanayohusu biashara ya kimataifa, fedha, na diplomasia ni mtu pekee aliyeweza kuonekana bora kuchukua wadhifa huu.

Na vile vile anaungwa mkono na kuheshimiwa na maafisa wengi duniani na pia anaamini kwa dhati lengo la benki ya Dunia la kupambana na umaskini.

Tayari mataifa ya ulaya yametoa maoni yao kuhusu uteuzi huo,waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Bernard Kouchner amesema Robert Zoellick anayetarajiwa kutangazwa rasmi kuwa kiongozi wa benki hiyo ya dunia baadae leo lazima arudishe imani ya watu katika suala la kupambana na umasikini.

Tangu jadi Marekani inamteua rais wa benki ya dunia lakini baadhi ya nchi wanachama wa benki hiyo na wabunge kadhaa wa Marekani wametoa mwito kwa utawala huo wa Marekani kukiweka wazi kinya’ng’anyiro hicho na kuvutia wagombea mbali mbali duniani baada ya sakata hii ya rushwa iliyomuandama Wolfowitz.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW