1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Roberta Metsola achaguliwa tena kuwa Spika wa Bunge wa Ulaya

16 Julai 2024

Bunge la Ulaya limemchangua tena, kwa kura nyingi Roberta Metsola kuendelea na wadhifa wa Spika wa Bunge hilo.Wakati huo huo hatima ya Rais wa sasa wa Halmashauri ya Ulaya Ursula von der Leyen bado haijajulikana.

Spika wa Bunge la Ulaya Roberta Metsola
Roberta Metsola Spika wa Bunge wa UlayaPicha: Philipp von Ditfurth/dpa/picture alliance

Katika kura iliyopigwa Jumanne 16.07.2024 katika Bunge la Ulaya, bibi Metsola ambaye ni Spika wa Bunge hilo, alichaguliwa tena na wabunge 562 kati ya 699 walioshiriki katika kupiga kura. Mwanasiasa huyo kutokkea Malta anatoka kwenye kambi kubwa kabisa ya vyama vya kihafidhina katika bunge la Ulaya.

Metsola ameutumikia wadhifa huo tangu mwaka 2022. Amesema Bunge la Ulaya linapaswa kuwa imara katika umoja ulio madhubuti. Amesema Wabunge wa Umoja wa Ulaya wanapaswa kupitisha maamuzi ambayo wananchi wanayataka.

Metsola ameahidi kuyashughulikia matatizo yanayowakumba wananchi wa barani Ulaya ikiwa pamoja na uhaba wa nyumba za bei nafuu na pia ameahidi kutekeleza sera sahihi ya uhamiaji.

Katikati: Spika wa Bunge la Ulaya Roberta Metsola Picha: Jean-Francois Badias/AP/picture alliance

Amesema bara la Ulaya  linapaswa kuwa mahala bora zaidi kwa kujenga usalama zaidi, na msingi  wa ulinzi utakaowapa watu usalama.

Wakati vita vinaendelea karibu sana na Umoja wa Ulaya, jumuiya hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwa pamoja na mkwamo wa kiuchumi na hali ya sintofahamu duniani. Viongozi wa jumuiya hiyo wanapaswa kupambana na mazingira hayo, ana kwa ana, baada ya kuchaguliwa mnamo mwezi Juni.

Wakati huo huo watu wanasubiri kwa hamu, iwapo rais wa sasa wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya,Ursula von der Leyen atachaguliwa tena hapo siku ya Alhamisi tarehe 18.07.2024 kuutumikia muhula mwingine wa miaka mitano. Kinyangànyiro hicho kinatazamiwa kuwa cha patashika. Mnamo mwaka 2019 alishinda kwa kura tisa tu.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der LeyenPicha: Dursun Aydemir/Anadolu/picture alliance

Mkurugenzi mshiriki wa Kituo cha Sera barani Ulaya Elizabeth Kuiper, amesema Ursula von Leyen atapaswa kuwapa Wabunge uhakika kwamba Umoja wa Ulaya hautaiacha njia ya kupunguza hewa ya kaboni ili kupambana na mabadiliko ya tabia nchi. Wabunge wengine wanamtaka apunguze sheria zinazohusu udhibiti wa mazingira.

Kambi ya vyama vya kihafidhina ya Ursula von der Leyen ya EPP, ina viti 188 na kwa hivyo kimsingi ingeliwezekana kufikia idadi ya viti 361 vinavyohitajika ili kuweza kuchaguliwa tena lakini wabunge kadhaa wamesema hawatampigia kura.

Bunge jipya pia litawachagua makamu wa rais 14, mchakato unaotarajiwa kuwa tata kutokana na kambi za vyama vya mrengo mkali wa kulia kufanikiwa kupata viti vingi katika uchaguzi uliofanyika mwezi Juni. 

Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban alipozuru UkrainePicha: NurPhoto/IMAGO

Katika hatua inayoashiria mivutano ndani ya Umoja wa Ulaya, hotuba ya waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban imeahirishwa. Orban amewakasirisha viongozi wenzake wa Umoja wa Ulaya kwa kufanya ziara nchini Urusi na China. Sababu rasmi iliyotolewa ya kuahirisha hotuba hiyo ni kujaa kwa ratiba ya upigaji kura.

Chanzo: AFP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW